Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mheshimiwa Mayeka Mayeka, ameishauri Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kushirikiana na Halmashauri za wilaya wakati wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu maboresho ya sheria mbalimbali nchini.
Akizungumza leo tarehe Agosti 6, 2025 wakati alipotembelea banda la Tume hiyo wakati wa maonesho ya Nanenane yanayoendelea viwanja vya Nzuguni Mkoani Dodoma , Mh. Mayeka alisema ofisi za halmashauri zina mtandao mpana wa kuwafikia wananchi, hivyo zinaweza kusaidia Tume kupata maoni ya watu wengi kutoka makundi mbalimbali ya jamii.
“Ni muhimu Tume ikazitumia halmashauri kama daraja la kufikia wananchi wengi, hasa walioko vijijini, ambao mara nyingi wanakosa fursa ya kutoa maoni yao kwenye mchakato huu muhimu wa kisheria,” alisema Mh. Mayeka.
Mhe.Mayeka aliongeza kuwa Sheria bora ni zile zinazotokana na ushirikishwaji wa wananchi kwa kiwango kikubwa, kwani zinakuwa zimezingatia changamoto, maoni na mahitaji halisi ya jamii.
Kwa upande wake Bi. Vicky Mbunde ambae ni Afisa Sheria kutoka Tume alisema wameupokea ushauri huo na wataendelea kuimarisha ushirikiano na halmashauri mbalimbali nchini ili kuhakikisha maoni ya wananchi wengi yanakusanywa kikamilifu.
Aidha Bi. Vicky amefafanua kwamba moja ya changamoto ambayo tume inakabiliana nayo ni bajeti ndogo ya utekelezaji wa majukumu yake.
" Tume ina jukumu la kupitia Sheria zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo ni zaidi ya 400, hivyo inahitaji bajeti ya kutosha katika utekelezaji, ambapo kila Sheria inapaswa kufanyiwa tathmini baada ya miaka mitano ili kutathmini iwapo malengo ya kutungwa Sheria hiyo yamefikiwa " Alisema Vicky.
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imekuwa katika mchakato wa marekebisho ya Sheria mbalimbali ili ziendane na wakati, changamoto za sasa na maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ujumla.