Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

MCHAKATO WA KUPITIA  SHERIA INAYOSIMAMIA UVUTAJI SHISHA NA TUMBAKU UMEAANZA - MANDEPO
28 Jul 2025
MCHAKATO WA KUPITIA...

MCHAKATO WA KUPITIA  SHERIA INAYOSIMAMIA UVUTAJI SHISHA NA TUMBAKU UMEAANZA - MANDEPO

TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) imeanza mchakato wa kupitia sheria inayosimamia masuala ya uvutaji shisha na tumbaku ili kuifanyia maboresho kwa lengo la kulinda afya za watumiaji.

 Hayo yameelezwa na Katibu Mtendaji wa tume hiyo,George Mandepo, wakati wa mahojiano na TBC redio jamii katika kipindi cha Jilawi kuhusu jinsi tume inavyotekeleza majukumu yake.

“Kuna suala la kuvuta sigara na pia kuna kitu kinaitwa shisha, vijana wengi wanapenda sana japo kuna athari za kiafya na kiuchumi sababu anapofanya hayo hawezi kufanya kazi za uzalishaji, sasa tume imeona kuna haja ya kupitia sheria inayosimamia masuala ya shisha na tumbaku,”alisema.

Mandepo alisema tume pia imebaini kuwepo kwa mmonyoko mkubwa wa maadili hususani kwa vijana ambao wamekuwa wakijihusisha katika mambo ambayo hayana tija kwa taifa kama vile kucheza michezo ya kubahatisha (kamari) na uvutaji tumbaku.

“Masuala yanayohusu maadili ambayo yapo kwenye haki jinai na haki madai, tume tumeshaanza mchakato kupitia sheria zinazogusa michezo ya kubahatisha ili tuone namna gani inalinda haki ya mtoto, unakuta mtoto anatoka shuleni anakwenda kwenye vibanda umiza kwenda ‘kubet’ hali inayosababisha wasiwe na maadili,’ alisema Mandepo.

Mandepo alisema Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania pia inafanya mchakato wa kupitia sheria zinazohusu ardhi kazi ambayo itaanza rasmi mwakani kwani kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi nchini.

Naye Mkuu wa Sehemu ya Mapitio ya Sheria, Christina Binal, alisema kwa kipindi cha 2024/2025 alisema LRCT imefanikiwa kufanya mapitio ya sheria mbalimbali hususani sheria za kampuni kwa ajili ya kuangalia mapungufu yanayoathiri ufanisi wa utekelezaji wa sheria hizo na kutoa mapendekezo kwa serikali.

Alisema tume pia imepitia sheria ya majina ya biashara lengo la mapitio hayo ni kuangalia namna gani sheria hizo zinaathiriwa, pia kuangalia namna itakavyoweza kutekezwa kwa  ufanisi na kutoa mapendekezo kwa serikali.

Binali alisema lengo la kufanya mapitio ya sheri hizo ni kuzifanya ziweze kutekelezeka na kufanya mazingira ya uwekezaji na biashara yanakuwa mazuri na hivyo kuwavuti wawekezaji nchini.

“Pia tume ilipitia sheria ya takwimu nchini sura namba 351 lengo kuweka mfumo wa kurahisisha upatikanaji wa takwimu katika mamlaka mbalimbali na kufanya iweze kupatikana katka mamlaka moja ambayo ingerahisisha na kuongeza ufanisi katika kukusanya taarifa ili kuweza kufikia malengo ya kitaifa,” alisema.

Binal aliongeza kuwa Tume ilifanikiwa kuptia sheria ya usuluhishi sura namba 15 lengo kuangalia mapungufu ya sheria hizo na kupendekeza namna bora  ya kuzifanya sheria hizo ziweze kutekelezeka kwa ufanisi.

Alisema lengo la kupitia sheria hiyo ni ili ziweze kufikia malengo ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za mashauri na muda, msongamano wa mashauri mahakamani  na hivyo kuchochea maendeleo ya sekta ya biashara na uwekezaji,” alisema.

Binal alisema pia Tume imepitia sheria ya utatuzi wa migogoro ya mikopo katika benki kwani kumekuwa na changamoto katika utatuzi wa migogoro hiyo.

“Tunacholenga hapa ni kuona namna bora ya kushughulikia migogoro ya mikopo katika benki  kwa haraka bila kuathiri masuala ya ukuaji uchumi  na hivyo kuongeza tija katika masuala ya kipato katka nchi na kwa mtu mmoja mmoja,” alisema.

Aidha, alisema Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya sheria mfano katika kampeni ya msaada wa sheria wa mama Samia, Mbagala Dar es Salaam na kutoa vipeperushi, majarida vipindi vy redio, na Tv  ambapo kwa kutumia njia hizo wananchi zaidi ya milioni tano wamefikiwa.

Kwa upande wake Saada Bushiri ambaye ni Mkuu wa Sehemu ya Udhibiti Ubora LRCT, akizungumzia kuhusu sheria ya ndoa alisema iko wazi kuhusisana na mgawanyo wa mali kwa wanandoa ambapo mwanadoa awe mwanaume au mwanamke ana haki ya kupata kile ambacho amechangia wakati wa ndoa yao.

“Wakati talaka shauri la ndoa linapokuwa mahakamani baada ya mahakama kutamka kuwa ndoa imevunjwa hatua inayofuata huwa ni mgawanyo wa mali na mambo mengine na mahakama katika kuangalia namna gani mali zitagawanywa huwa inajikita kuangalia kiwango cha mchango cha mwanandoa huyo kama ilikuwa ni asilimia 20 itakuwa hivyo,” alisema.

Bushiri alisema wengine wamekuwa wakidhani mwanandoa akiwa mama wa nyumbani hana haki ya kupata mgawanyo wa mali, hapana, mama wa nyumbani ana haki kwenye mgawanyo wa mali sababu anakuwa amemsaidia mwenzake katka kutekeleza majukum yake ya kutafuta kipato katika familia.

Mwisho