Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

LRCT YATOA ELIMU YA SHERIA YA UMWAGILIAJI NIRC.
05 Aug 2025
LRCT YATOA ELIMU YA...

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) imetoa elimu kuhusu Sheria ya Tume ya Umwagiliaji kwa watumishi wa Tume ya Umwagiliaji nchini, wakati wa Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

Elimu hiyo imetolewa leo tarehe Agosti 5, 2025 na mawakili kutoka Tume ya Kurekebisha sheria Vicky Mbunde na Baraka Chipamba wakati wa maonesho ya Nanenane walipotembelea moja ya ofisi ya tume hiyo iliopo Nzuguni katika viwanja hivyo vya maonesho, ikiwa ni sehemu ya juhudi za LRCT kuhakikisha watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla wanaelewa sheria zinazowaongoza katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Katika maelezo yake kwa watumishi hao, Wakili Baraka Chipamba alisema kuwa Sheria ya Tume ya Umwagiliaji ni msingi muhimu wa usimamizi wa rasilimali za umwagiliaji nchini, na ni wajibu wa kila mtumishi kuielewa ili kuepusha migongano ya kiutendaji na kuboresha utoaji wa huduma.

“Sheria hii inaweka misingi ya kiuendeshaji wa Tume ya Umwagiliaji, ikiwa ni pamoja na majukumu, mipaka ya madaraka, uwajibikaji na namna bora ya kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo,” alisema Baraka.

Watumishi wa Tume ya Umwagiliaji walipata fursa ya kuuliza maswali na kujadili changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao kwa mujibu wa sheria ambapo Bw. Petro Lawaisa Afisa Kilimo Mwandamizi Tume ya Umwagiliaji ameeleza kuwa uelewa mdogo wa baadhi ya wanavijiji kuhusu sheria ya umwagiliaji na haki zao katika miradi ya umwagiliaji imekuwa ni changamoto kubwa katika maeneo mengi nchini.

Aidha ameiomba Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kuipitia sheria ya Tume ya Umwagiliaji ili kuona kama inaweza kutatua changamoto ya ulipiaji wa huduma na miundombinu ya umwagiliaji jambao ambalo limekuwa ni changamoto kwa wananchi wengi.

Kwa upande wake Wakili Vick Mbunde wa LRCT alihimiza watumishi hao kuendelea kusoma na kufuatilia mabadiliko ya sheria zinazohusu sekta yao, huku akiweka wazi kuwa LRCT iko tayari kupokea mapendekezo kutoka kwao kuhusu maeneo ya sheria yanayohitaji kufanyiwa marekebisho au maboresho.

Tume ya Kurekebisha Sheria imekuwa ikitumia jukwaa hilo kuelimisha wananchi kuhusu sheria mbalimbali, ikiwa ni pamoja na zile za ardhi, maji, kilimo na haki za kijamii.