Menejimenti ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) imekutana katika kikao kazi maalum na timu ya wasimamizi wa mali za Serikali kutoka Wizara ya Fedha ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa mali na utekelezaji wa majukumu ya usimamizi wa rasilimali za Umma ndani ya taasisi hiyo ya kiserikali.
Kikao hicho, kilichofanyika katika ofisi za Tume Jijini Dodoma, kililenga kupitia taarifa za mali za Tume, kuimarisha usimamizi wa rasilimali, na kujadili changamoto mbalimbali zinazokumba utekelezaji wa sera na miongozo ya usimamizi wa mali za Serikali.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume, Bi. Juliana Munisi, aliwahakikishia Wasimamizi wa mali za serikali kuwa Tume inaendelea kusimamia wajibu wake wa kisheria na kiutawala katika kusimamia mali za Umma kwa uadilifu na uwazi. Alieleza kuwa kikao hicho ni fursa muhimu ya kufanya tathmini ya mwenendo wa usimamizi wa mali na kuhakikisha kuwa Tume inazingatia kikamilifu miongozo ya Wizara ya Fedha na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Tume inathamini kazi ya uhakiki mali kwani inatusaidia kubaini maeneo yenye mapungufu, kuimarisha mifumo yetu ya udhibiti wa ndani, na kuchukua hatua stahiki kwa wakati,” alisema Bi Juliana
Kwa upande wao, wahakiki mali kutoka Hazina wakiongozwa na Bi. Winfrida Kalinga na Margareth Kaiza walisema kuwa zoezi hilo ni sehemu ya jukumu endelevu la kuhakikisha kuwa taasisi zote za Umma zinafuata taratibu na miongozo iliyowekwa kuhusu usimamizi wa mali za Serikali. Alibainisha kuwa uhakiki huo unahusisha kupitia vielelezo, kutembelea mali halisi, na kujiridhisha kuhusu usahihi wa taarifa zinazowasilishwa katika vitabu vya hesabu.
"Tunalenga kuhakikisha kuwa mali zote zilizonunuliwa na Serikali kupitia Tume hii zimesajiliwa, zinatunzwa ipasavyo, na taarifa zake zinapatikana kwa uwazi,” alisema Bi. Winfrida Kalinga
Tume iliahidi kushirikiana kwa karibu na Hazina kuhakikisha kuwa mapendekezo yote ya ukaguzi na uhakiki yanatekelezwa ipasavyo
Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha uwajibikaji na ufanisi katika usimamizi wa mali za Umma, sambamba na azma ya kuhakikisha kuwa kila taasisi inafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.