Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakimu Maswi, amewataka watumishi wa Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania kuongeza ubunifu na kutumia maarifa mapya katika kutekeleza majukumu yao ili kuongeza ufanisi na kuendana na mabadiliko ya kiutendaji ndani ya Serikali.
Maswi alitoa wito huo tarehe 19/11/2025 wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi uliofanyika katika Hoteli ya Sanaan, Jijini Dodoma, Kikao kilichowakutanisha wajumbe wa baraza la wafanyakazi watumishi mbalimbali kutoka ngazi mbalimbali za TUGHE Taifa na Mkoa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Maswi alisema Tume ina nafasi muhimu katika uimarishaji wa misingi ya utawala bora, hivyo watumishi wanapaswa kuongeza ubunifu katika utatuzi wa changamoto, utafiti , na utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Watumishi lazima wabuni mbinu mpya za kufanya kazi, kutumia teknolojia ipasavyo, na kufikiri nje ya mipaka ya kawaida. Ubunifu ndiyo msingi wa kuongeza matokeo na kuboresha huduma kwa wananchi,” alisema Maswi.
Aliongeza kuwa ubunifu si jukumu la idara fulani tu, bali ni wajibu wa kila mtumishi, kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu. Alisisitiza kuwa Serikali inategemea mawazo mapya kutoka kwa watumishi wake ili kuharakisha maboresho ya mifumo ya sheria na haki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Bw. George Mandepo alieleza kwamba Tume kwa mwaka wa fedha 2025/26 imejipanga kufanya utafiti juu ya mfumo wa sheria zinazohusiana na biashara ya jewa ukaa, utafiti kuhusu mfumo wa sheria zinazoehusiana na teknolojia ya akili unde na mapitio ya sheria ya Bima za magari sura ya 169.
Aidha, kazi nyingine ni mapitio ya sheria ya bima sura 394 na mapitio ya sheria iliyoanzisha Tume ya kurekebisha sheria Tanzania sura ya 171 alieza Mandepo
Hata hivyo Bw. Mandepo alisema Tume kwa kushirikiana ofisi ya mwanashria mkuu wa Serikali na Wizara ya Katiba na sheria wameunda kikosi kazi ambacho kinaendelea na uchambuzi wa sheria za kipaumbele na uandaaji wa bajeti kwa ajili ya utekelezaji ili kuhakikisha Dira inafikia malengo tarajiwa.