Kamishna wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Bw. Iddi Mandi, ametoa wito kwa wataalamu na watafiti wa tume hiyo kuhakikisha kuwa wanapata maoni ya wananchi wa kawaida wakati wa tafiti wanazozifanya ili kuhakikisha maboresho ya sheria yanayopendekezwa yaweze kuwa na manufaa kwa jamii nzima.
Akizungumza wakati wa wasililisho lake kuhusu utafiti wa Kisheria kwa wajumbe wa Baraza la wafanyakazi la Tume hiyo lilofanyika leo tarehe 18. /11/2025 katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Saanan Jijini Dodoma, Bw. Mandi alisema kuwa tafiti nyingi za kisheria zinapoishia kufanywa kwenye Taasisi, Wizara mbalimbali na watu mashuhuri, hupunguza uhalisia wa changamoto zinazowakabili wananchi wengi wanaoishi katika maeneo ya pembezoni na miji.
“Ni muhimu tafiti zetu ziwe za kina na zenye uwakilishi mpana. Tunapaswa kuwafikia wananchi wa kawaida, maana wao ndio wahanga wakuu wa sheria tunazozifanyia marekebisho. Hatutaki sheria zinazobaki kwenye makaratasi bila kuwa na uhalisia kwenye maisha ya watu,” alisema Bw. Mandi.
Amesisitiza kuwa ufanisi wa tume hiyo unategemea uwezo wake wa kuwasikiliza wananchi, kuelewa mahitaji yao, na kuyatumia kama msingi wa mapendekezo ya mabadiliko ya sheria.
Kwa mujibu wa Kamishna Mandi, tafiti za kisheria zinapaswa kuwa chombo cha kuhakikisha haki inatendeka na kwamba sheria zinakidhi mahitaji ya kizazi cha sasa bila kupoteza misingi yake ya kulinda maslahi ya umma.
Bw. Mandi ameitaka timu ya utafiti ya tume hiyo kubuni mbinu shirikishi, ikiwemo kufanya mikutano ya hadhara, kutembelea vijiji na vitongoji, pamoja na kuendesha majadiliano na makundi mbalimbali ya jamii ili kupata maoni mapana kabla ya kuandaa mapendekezo rasmi ya marekebisho ya sheria.
Tume ya Kurekebisha Sheria inaendelea na mchakato wa mapitio ya sheria mbalimbali nchini, ambapo ushiriki wa wananchi umetajwa kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha marekebisho yenye tija na yanayotekelezeka.
Kikao cha Baraza la wafanyakazi Tume ya Kurekebiha Sheria Tanzania kilihudhuriwa na wajumbe kutoka idara mbalimbali za tume hiyo na wageni kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) taifa na Mkoa.