Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

JAMII IKIJUA ADHABU ZITOKANAZO NA MAKOSA YA MAADILI ITABADILIKA.
28 Apr 2025
JAMII IKIJUA ADHABU...


Wanafunzi wanaosoma Shule ya Sekondari Lindi (Lindi High School) na Shue ya Sekondari ya  Lindi  Wasichana mkoani humo, walisema adhabu zilizoanishwa kwa  mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ni kali hivyo  zinaweza kua kinga madhubuti katika kudhibiti mmomonyoko wa maadili nchini.

Wanafunzi hao wameleeza hayo tarehe 28/4/2025 mkoani Lindi walipokua wakijengewa uwezo kuhusu Sheria mbalimbali hususan makosa ya kimaadili. Mada ambazo ziliwasilishwa na Wanasheria kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania. 

Wakizungumza mara baada ya kujifunza makosa ya maadili kwa kuainishiwa kila kosa na adhabu kwa atakaethibitika kutenda makosa hayo, Feisal Hamidu na Cecilia Paul ambao ni wanafunzi wa shule ya Sekondari Lindi walisema hawakuwahi kufahamu kabla kuwa makosa ya kimaadili yana adhabu kali na kuahidi  kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha wengine kutokutenda makosa hayo yanayokwenda kinyume na sheria.

“Kwa mfano mimi sikua nafahamu kama kuna maneno, ishara au sauti unaweza kufanya kwa mtu kama utani lakini  ikawa ni udhalilishaji  kwa mujibu wa Sheria: alisema Feisal  

Sambamba na hilo mwanafunzi ,Leila Ramadhan anaesoma Shule ya Sekondari Lindi Wasichana alisema elimu hiyo imesaidia kujua sehemu sahihi za kuripoti matukio ya kimaadili akibainisha kuwa manusura wa makosa hayo wengi  ni wasichana hasa katika matendo ya ubakaji, ulawiti,na utoaji mimba nakuhaidi kuwa balozi mzuri  katika kuwaelimisha wengine kujua haki na wajibu wao kwa mujibu wa sheria.


Kwa upande wake Mwalimu, Farida Saidi Majid ambaye ni Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Lindi alisema kitendo cha wanafunzi kujifunza na kuelewa kuhusu makosa ya kimaadili na adhabu zake zimewatia hofu wanafunzi na kwamba watakua mabalozi wazuri kwa wengine na hii kuifanya Lindi kuwa na watu wenye kuzingatia maadili mema.

Afisa Sheria kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Bi Jackline Nungu alisema dhumuni la mafunzo hayo ni kujenga uwelewa wa masuala ya kisheria kwa jamii, lakini pia kuwaonesha wanajamii jinsi wanavyoweza kupata matatizo pindi watakapotenda kinyume na Sheria, akitolea mfano wa adhabu ya baadhi ya makosa  kama ubakaji ni kifungo gerezani kuanzia miaka 30 hadi maisha, faini na fidia kwa manusura.

Jackline alisema wanajamii wakijua adhabu ya makosa mbali mbali itasaidia kujihadhari kutotenda makosa hayo, lakini pia elimu hiyo inapowafikia inasaidia kukumbusha jamii wajibu wao wa kutii sheria bila shuruti.

“Masomo haya ni ya muhimu katika jamii na Tume inaendelea kutekeleza jukumu hili kama majukumu yake yalivyoainishwa katika Sheria ya kuanzishwa kwa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania”. Alimaliza kwa kueleza Jackline.