Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

ELIMU YA SHERIA YA MAADILI YAWAFIKIA WANAFUNZI SHULE YA SEKONDARI YA WASICHANA MTWARA
28 Apr 2025
ELIMU YA SHERIA YA M...

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara (Mtwara Girls High School) wameaswa kutojihusisha na vitendo vya ukiukaji maadili kwani kufanya hivyo kunaweza kukatisha ndoto zao pale itakapobainika kisheria kuwa wametenda makosa yatakayowatia hatiani.

Hayo yameelezwa tarehe 25/4/2025 na Afisa sheria kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bi. Jackline Nungu alipokuwa akitoa elimu ya Sheria kuhusu Makosa ya Maadili kwa wanafunzi hao wa Shule ya Wasichana Mtwara.

Jackline aliwataka wanafunzi hao kujihadhari na matendo yaliyo kinyume na maadili kama vile, mahusiano ya jinsia moja, kufanikisha ubakaji, udhalilishaji wa kingono, kutumikisha watoto kingono, shambulio la aibu, kufanikisha kutoa mimba na utoaji mimba na mengineyo .Bi. Jackline alieleza adhabu za makosa hayo ni kifungo, faini au vyote kwa pamoja kulingana na mazingira ya utendaji wa kosa. Vilevile alisisitiza kutokujua Sheria haiwezi kuwa sababu ya kutokutiwa hatiani itakapothibitika umetenda kosa kisheria” alisema Jackline

Awali Naibu Katibu Mtendaji wa Kitengo cha Elimu ya Sheria kwa Umma Bi. Zainab Chanzi aliwaeleza wanafunzi hao kuhusu majukumu ya Tume ya Kurekebisha  Sheria Tanzania kuwa ni kufanya Mapitio na Tathmini ya Sheria zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na kutoa Elimu ya Sheria kwa Umma. Aidha, aliwaeleza wanafunzi hao lengo la kufika shuleni hap ni kuwajengea uwezo na uelewa kuhusu masuala ya kisheria.