Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

DCS ATEMBELEA KAMBI YA TUMESHERIA SPORTS CLUB JIJINI MWANZA.
06 Sep 2025
DCS ATEMBELEA KAMBI...

Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi (DCS) Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Bw. Mohamed Mavura, ametembelea kambi ya wanamichezo wa timu ya Tumesheria Sports Club wanaoshiriki michuano ya SHIMIWI 2025 inayoendelea Jijini Mwanza.

Bw. Mavura ametembelea kambi hiyo iliyojichimbia Kiloleli Manispaa ya Ilelema, tarehe 6 Septemba 2025 na kuzungumza na Viongozi wa timu pamoja na wachezaji wa timu hiyo ikiwa ni sehemu ya kuwapa motisha kuelekea michezo iliyo mbele yao. Akizungumza katika kikao kifupi na wachezaji alipowasili kambini hapo, Bw.Mavura ameipongeza timu ya Tumesheria sports Club, kwa kufanikiwa kufika hatua ya 16 bora ya mashindano ya kuvuta kamba Wanawake.

Vile vile amewataka kuongeza bidii ili wafike Fainali na hatimae wachukue Kombe la Ushindi wa michuano hiyo.

"Tukiangalia tulipotoka katika michuano hii ya SHIMIWI nadhani sasa tunaimarika kutoka miaka iliyopita hadi sasa", alisema Bw.Mavura

Aidha amesisitiza wanamichezo hao kuzingatia mazoezi, kuendelea kuwa na ushirikiano na mshikamano na kupeana msaada na kuwataka wachezaji kujenga tabia ya kuishi pamoja katika kambi ili kuimarisha nidhamu katika kipindi chote cha mashindano.

"Msiache kushirikiana miongoni mwenu. imarisheni kambi kwa kuweka nidhamu kubwa na hasa sisi tunasubiri kombe mrudi nalo" alisisitiza Bw.Mavura.

Awali Mwenyekiti wa Tumesheria Sports Club, Msafiri Shamsi akiongea kwa niaba ya wachezaji amemshukuru Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bw. George Mandepo, kwa kuendelea kuwapa nafasi ya kushiriki na kutoa kipaumbele katika michezo ya SHIMIWI.

Nae Nahodha wa timu ya kuvuta kamba Wanawake Tumesheria Sports Club Bi. Sarah Lukambinga alieleza kuhusu timu yao na wachezaji walivyo imara na walivyojipanga katika kukabiliana na wapinzani watakaopangwa nao hatua zijazo ili kupata matokeo mazuri.

Michuano ya SHIMIWI 2025 inaendelea Jijini Mwanza kwa michezo mbalimbali ikiwemo kuvuta kamba, baiskeli, karata, bao, mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha,kurusha tufe na mingineyo ambapo ilianza rasmi tarehe 1 Septemba 2025 na inategemewa kuhitimishwa tarehe 16 Septemba 2025.