Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

TUME YAWEKA RAMANI YA UTEKELEZAJI WA MABORESHO YA SHERIA KWA MIAKA MITANO ILI KUFANIKISHA DIRA 2050.
21 Jun 2026
TUME YAWEKA RAMANI Y...

Katibu Mtendaji Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Bw. George Mandepo, amebainisha kwamba Tume hiyo kwa kushirikiana na wadau wa Taasisi za Maboresho ya Sheria imeandaa andiko la programu ya maboresho ya Sheria pamoja na ramani ya utekelezaji (Road Map) kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2026/2027 hadi 2030/2031 kwa lengo la kuwezesha utekelezaji kamili wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Bw. Mandepo amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa wakati wa uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mfumo wa sheria unaoendana na mahitaji ya maendeleo ya taifa katika kipindi cha miongo ijayo.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa Mkutano wa Wadau wa Taasisi za Maboresho ya Sheria uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya APC Bunju, mkoani Dar es Salaam, Bw. Mandepo alisema programu hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya taifa pamoja na mabadiliko yanayotokea katika nyanja mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kiteknolojia.

Alifafanua kuwa ramani ya utekelezaji iliyotayarishwa itaongoza hatua mbalimbali za maboresho ya sheria kwa kipindi cha miaka mitano, huku ikibainisha maeneo ya kipaumbele yatakayofanyiwa mapitio ili kuhakikisha sheria za nchi zinachochea maendeleo endelevu na mazingira bora ya uwekezaji, biashara na utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Maandalizi ya Programu ya maboresho ya sheria na ramani ya utekelezaji yamehusisha wadau mbalimbali ili kuhakikisha kunakuwa na uelewa wa pamoja na ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yanayolenga kuimarisha mfumo wa sheria nchini,” alisema Bw. Mandepo.

Amesema kwa kuzingatia umuhimu na Watafiti kuwa na uelewa wa kina kuhusu mifumo ya Sheria tmbalimbali zitafanyiwa  tafiti na mapitio, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania pamoja na wadau wa Kundi Na. 4 kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipango imeandaa mafunzo kuhusu Mfumo wa Sheria za Nishati na Mfumo wa Sheria za Viwanda, Biashara, na Uwekezaji kwa washiriki ambao watashiriki katika kufanya tafiti na mapitio ya Sheria hizo.

Ameeleza kwamba mafunzo hayo yanalenga kujenga uelewa wa pamoja, kubadilishana uzoefu, na kuweka mikakati thabiti ya kufanya tafiti na kufanya mapitio ya Sheria za Nishati, Viwanda, Biashara, na Uwekezaji nchini Tanzania ili kuzifanya ziendane na Dira 2050 kama maelekezo ya Mhe. Rais yalivyoelekeza.

Aidha, alieleza kuwa ushiriki wa wadau katika mchakato huo umewezesha kukusanywa kwa maoni na mapendekezo muhimu yatakayosaidia kuimarisha ubora wa programu hiyo na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wake.

Akichangia mada hiyo, Dkt. Suleiman Serera alisema maandalizi ya Programu ya Maboresho ya Sheria na Ramani ya Utekelezaji ni hatua muhimu katika kuhakikisha mfumo wa sheria nchini unaendana na maono na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Dira 2050 imeweka matarajio makubwa ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia. Ili kuyafikia, ni lazima tuwe na sheria zinazokwenda sambamba na mabadiliko hayo. Hivyo, programu hii inatoa mwongozo wa maeneo ya kipaumbele yatakayofanyiwa maboresho ili kuhakikisha sheria zetu zinakuwa kichocheo cha maendeleo badala ya kuwa kikwazo,” alisema Dkt. Serera.

Hata hivyo, aliwataka wadau kuendelea kutoa ushirikiano na maoni yenye kujenga ili kuhakikisha Programu ya Maboresho ya Sheria inatekelezwa kikamilifu na kuleta matokeo chanya katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.