Habari
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Kutupia Jicho Sheria ya Takwimu
Kamisheni ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (Law Reform Commission of Tanzania - LRCT) leo tarehe 21.10.2024 imekutana mjini Morogoro kujadili utekelezaji wa kazi ya mapitio ya Sheria ya Takwimu, Sura ya 351 ili kuiboresha na kuifanya iendane na wakati uliopo .
Akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa jukumu hiloKatibu Mtendaji waTume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bw. George Mandepo amesema kwamba Tumeimepewa jukumu la kufanya mapitio ya Sheria hiyoili kupendekeza maboresho kwa serikali.
“Tume ilifanya mapitio haya kwa njia ya utafiti pamoja na majadiliano na wadau mbalimbali, ili kupata maoni yao kwa ajili ya kutoa mapendekezo ya kisheria nay a kiutawala kwa serikali yatakayosaidia kuboresha Sheria husika’.
Kuhusu Sheria hiyo ya Takwimu, Bw. Mandepo alifafanua kwamba Tume imeweza kupendekeza marekebisho ili kuhakikisha kuwa sheria hiyo inaendana na mahitaji ya sasa na hali ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi, na kisayansi nchini.
Bw. Mandepo amesema kuwa Sheria ya Takwimu ni muhimu kwa sababu inasimamia uzalishaji, ukusanyaji na usambazaji wa takwimu rasmi nchini ikiwemo takwimu za kiutwala ambazo ni muhimu katika kupanga sera, kutathmini maendeleo, na kufanya maamuzi.
Hata hivyo alibainisha kwamba mapitio ya Sheria hiyo yamejumuisha viini mbalimbali vya utafiti kama vile Uhuru wa taasisi kaktika kuzalisha na kusambaza takwimu na kuhakikisha kuwa takwimu zinazokusanywa zinapatikana kwa urahisi na usahihi kwa watumiaji wote, ikiwemo watafiti, wawekezaji, na wananchi kwa ujumla alifafanua Mtendaji huyo Mkuu wa Tume.
Aidha Bw.Mandepo ameeleza kwamba maboresho ya sheria hiyo yatasaidia ulinzi wa faragha na usalama wa taarifa na uwajibikaji wa taasisi zinazokusanya takwimu ili kuimarisha ubora wake na uaminifu katika takwimu zinazozalishwa.
“Mapendekezo yaliyotolewa yataimarisha mifumo ya kisheria inayohusiana na ulinzi wa data binafsi, ili kuhakikisha kwamba taarifa za wananchi zinafichwa na kulindwa dhidi ya matumizi mabaya”. Alisema Mandepo
Vilevile, amefafanua kwamba Sheria ya Takwimu itachangia uwezeshaji wa teknolojia na ubunifu kwa kuweka mazingira bora kwa matumizi ya teknolojia za kisasa katika ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu.
Bw. Mandepo alibainisha kwamba kwa kufanya mapitio hayo, Sheria ya Takwimu Nchini Tanzania itakuwa na uwezo wa kusaidia maendeleo endelevu na kutoa taarifa sahihi kwa ajili ya uamuzi bora katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kijamii.