Habari
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) na Tume ya Kurekebisha Sheria na Maendeleo ya Namibia wakutana Dodoma kubadilishana uzoefu .
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania LRCT Leo tarehe 20/09/2024 imetembelewa na Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria na Maendeleo ya Jamhuri ya watu wa Namibia Bw. Etuna Joshua kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi wao wa Kila Siku.
Wakiongea wakati wa mkutano uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Tume hiyo ulioko katika majengo ya Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) wamesema Tume hizo zinafanya kazi zinazofanana lakini zinatofautiana katika mambo machache yakiwemo idadi za taarifa kwa mwaka na rasilimali watu na fedha.
Akiongea wakati wa mijadala mbalimbali Dkt. Iddi Ramadhani Mandi wa kamisheni ya Tume hiyo ameeleza kwamba Tume hizo zinakabiliwa na changamoto ya rasilimali watu na fedha za kutosha kufanya utafiti Kila zinapohitajika.
Amesema pande zote zinaona umuhimu wa uwepo wa matumizi ya Teknolojia za kisasa za ukusanyaji wa taarifa kwa wananchi ili kufanya miradi mingi kwa muda mfupi.
Awali akielezea namna LRCT inavyofanya kazi Dr. Mandi amefafanua kwamba Sheria zinazofanyiwa utafiti na Tume hiyo zinakuwa haziegemei upande wowote na zinadumu kwa muda mrefu bila kuhitaji maboresho.