Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

Habari

TUME IMEANZA KUFANYA UTAFITI NA TATHMINI YA SHERIA ZA MAKOSA DHIDI YA MAADILI.


Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeanza rasmi kufanya utafiti na mapitio ya sheria zinazosimamia makosa dhidi ya maadili kwa kuwakutanisha wakuu wa upelelezi wa jinai Tanzania Bara na Zanzibar na waendesha mashtaka wa mikoa ya Tanzania bara. Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Bunge na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuiagiza Wizara ya Katiba na Sheria kutokana na kuwepo kwa ongezeko la kasi ya vitendo vya mmomonyoko wa maadili nchini.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Ndg.Griffin Mwakapeje alipokuwa akitoa ufafanuzi jana tarehe 12 Mei 2023.jijini Dodoma jana wakati wa kikao kazi cha kukusanya maoni ya mapitio ya sheria zinazosimamia makosa dhidi ya maadili Tanzania kilichowakutanisha wakuu wa upelelezi wa jinai Tanzania Bara na Zanzibar na waendesha mashtaka wa mikoa yote nchini kilichoandaliwa na Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Aidha, akizungumza kwenye mkutano uliowakutanisha wataalamu hao, Katibu Mtendaji wa Tume, Griffin Mwakapeje alisema tayari taratibu za ndani zimekamilika na kwa mara ya kwanza wamekutana na wakuu wa upelelezi wa jinai na waendesha mashtaka wa mikoa kwa lengo la kupata taarifa na takwimu za makosa hayo nchini.

“Pia tunataka kuangalia changamoto za kisheria wanazokabiliana nazo katika ukamataji, upelelezi na uendeshaji wa mashauri hayo mahakamani. ”Alisema timu ya Tume ambayo imejumuisha wataalamu na wabobezi kwenye maeneo mbalimbali itaendelea katika mikoa mbalimbali kuanzia Mei 17 mwaka huu ili kukutana na makundi yatakayosaidia kupata taarifa na takwimu za makosa ya kimaadili.

Makosa dhidi ya maadili ni pamoja na kubaka, genge la ubakaji, kujaribu kubaka, kuteka, udhalilishaji wa kingono, kuwaingilia kingono watu wenye ugonjwa wa afya ya akili, kumuingilia mtu asiye mke mwenye umri chini ya miaka 18 bila ridhaa yake, kuwatweza watoto kingono.

Vilevile makosa ya udhalilishaji mkubwa wa kingono, uwakala wa ukahaba, kumiliki madanguro, kuingilia kinyume na maumbile(ushoga), kuzini na maharimu, kusambaza picha za ngono, ponografia kwa watoto na kwa njia ya mtandao, usagaji na mengine yanayofanana na hayo.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitula alisema hadi jana mashtaka ya mmomonyoko wa maadili yakihusisha vitendo vya ulawiti, ubakaji na mengine ambayo yapo katika wilaya ya Kigamboni ni karibu asilimia 40 hivyo tatizo bado ni kubwa.

Alisema ofisi ya DPP kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wamekuwa wakisimamia makosa ya jinai kwa upelelezi na namna ya uendeshaji wake. “Ni ukweli usiopingika kwamba kumekuwa na ongezeko la makosa haya yanayogusa maadili katika nchi yetu ikiwemo ulawiti, ubakaji na mengine ya ukatili wa kijinsia.”

“Makosa haya yapo nchi nzima, japo kuna mikoa na sehemu chache yanaonekana yapo zaidi, lakini ni tatizo kubwa kwa taifa letu.”

“Katika Wilaya ya Kigamboni mashtaka ambayo yapo Mahakamani karibu asilimia 40 ni ya namna hii, kwahiyo mnaweza kuona namna ambavyo tatizo ni kubwa.” Mwakitalu alisema kikao hicho ni muhimu sana kwa sababu kitatoa mwanga na kuonyesha njia ya kupata ufumbuzi wa namna bora ya kukabiliana na majanga ya namna hiyo ambayo yanalikabili taifa. “Niwaombe washiriki tujadili kwa wazi na kina, kwa sababu maazimio ya kikao kazi hiki yatakuwa na matokeo chanya kwenye kutuwezesha kupata sheria bora zinazosimamia maadili katika nchi yetu.” Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai ambaye ni Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Salehe Ambika aliwataka waendesha mashtaka hao na wakuu wa upelelezi kutoa taarifa kwa uwazi, maoni na mapendekezo ili kama sheria zilizopo zina changamoto zifanyiwe marekebisho.