Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

Habari

TATHMINI IFANYIKE KWA SHERIA ZINAZOSIMAMIA MAKOSA YA MAADILI- MARY MAKONDO


Akifungua mkutano wa 18 wa baraza la wafanyakazi la tume hiyo siku ya tarehe 14 mwezi machi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo alisema masuala ya maadili yanapaswa kuangaliwa kwa tume kufanya tathmini.

Alisema kwa kufanya hivyo wataona kitu gani kifanyike katika maboresho ya Sheria lakini pia adhabu ambazo zinapaswa kuendana na masuala ya uvunjifu wa maadili nchini.

“Ni suala ambalo wote tushirikiane ili tuweze kupata matukio kwa haraka. Nasema hivyo kutokana na kuwepo kwa vitendo vingi sana kwa siku za hivi karibuni vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo makosa makubwa ya ubakaji, ulawiti pamoja na udhalilishaji wa wanawake na watoto, ”

Mary alisema watu wamekuwa wakisikia matukio hayo yakijitokeza majumbani, shuleni na kwamba inasikitisha wakati mwingine wahusika ni sehemu ya familia.

Aliwataka wazazi na walezi kuwajibika ipasavyo katika eneo la malezi kuanzia nyumbani na mahali popote ili kulinda Taifa na kwamba watanzania wote wanawajibu wa kushirikiana ili kudhibiti ukiukwaji ama udhalilishaji wa maadili kwa wanawake na watoto.

Kauli hiyo imekuja wakati nchi ikikabiliwa na changamoto ya matukio ya kikatili ikiwemo mauaji, ulawiti, ubakaji na udhalilishaji wa wanawake na watoto.

Aidha, Mary aliitaka tume hiyo kuongeza muda wa kupokea maoni juu ya maboresho ya sheria mbalimbali yanayoendelea nchini hadiMachi 30 mwaka huu ili kuwezesha wananchi wengi kuwasilisha maoni yao. “Hii itasaidia dhana ya ushirikishwaji mpana zaidi katika maendeleo ya Taifa ikiwemo eneo mahususi la mapitio na maboresho ya sheria zetu nchini,”alisema.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya kurekebisha sheria Bw.Griffin Mwakapeje alisema katika mwaka huu wa fedha tume imefanikiwa kufanya yafuatayo:

(a)Kukamilisha Mapitio na Utafiti wa Mfumo wa Sheria na kuandaa taarifa 8 ambazo ziliwasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana;

(b) Kuandaa na kuwasilisha kwa Waziri mwenye dhamana taarifa ya awali ya Mapitio kuhusu Mfumo wa Sheria Unaosimamia Uchaguzi na Vyama vya Siasa nchini Tanzania; na

(c)Kukamilisha Ripoti ya Mapitio Kuhusu Mfumo wa Sheria Unaosimamia Utoaji Haki katika Mahakama za Mwanzo.

Kwa upande wa Utafiti na Tathmini ya Sheria, Tume imeandaa maandiko ya tathmini ya Utekelezaji wa Sheria mbalimbali kwa lengo la kubaini endapo malengo yaliyokusudiwa kwa kutungwa kwa Sheria hizo yamefikiwa. Kwa sasa Tume inajiandaa kukutana na wadau mbalimbali wakiwemo watekelezaji wa sheria hizo kwa lengo la kupata maoni yatakayowezesha kutoa mapendekezo.

Sambamba na hayo, katika mwaka huu pia, Tume imeona vema kuwashirikisha wananchi, ambao mwisho wa siku ndio watumiaji wa sheria, kuandaa mpango wa mapito wa sheria mbalimbali ambao zinaonekana kuleta changamoto ndani ya jamii. Lengo la ushirikishwaji huu, pamoja na mambo mengine, ni kutimiza masharti ya sheria iliyoianzisha Tume lakini pia kutekeleza kwa vitendo falsa ya Mheshimiwa Rais ya Maridhiano (Reconciliation), ustahimilivu (Resilience), Mabadiliko/maboresho/Marekebisho (Reform) na kujenga (Rebuild).

Tume imewaomba wananchi wote kushiriki katika mpango huu ili wawe sehemu kubwa ya maboresho na marekebisho ya sheria yanayoendelea kufanywa ndani ya nchi. Naomba kutumia fursa hii kuwashukuru Wananchi wote waliojitokeza pamoja na baadhi ya Wizara na Taasisi zilizowasilisha maoni ili tukamilishe Mpango wa Mapitio ya Sheria wa 2023/2025.Mheshimiwa Mgeni Rasmi

Hadi sasa ni Wizara Nne tu (4) zilizotoa na kuwasilisha kwetu maoni: nazo ni Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira): Wizara ya Mifugo na Uvuvi; Wizara ya Viwanda na Biashara; na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Aidha, Taasisi zilizowasilisha maoni ni pamoja na Tume ya TEHAMA; Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO); na TUCTA. Kati ya Wananchi 1761 waliotembelea Tovuti ya Tume, 240 wametoa maoni yao na mwananchi mmoja amewasilisha kwa maandishi. Maoni haya tutayachambua na kuandaa Mpango uliokusudiwa tayari kuanza kuufanyia kazi.

Tume inawaomba na kuwasihi wananchi na taasisi ambazo bado hazijaitumia fursa na haki yao ya kikatiba ya kutoa maoni, wayatoe ili tuboreshe na kurekebisha sheria zetu kwa manufaa na maendeleo yetu sote. Maoni hayo yanatolewa kupitia tovuti ya Tume www.lrct.go.tz kwenye sehemu ya eneo la karibu na kubofya palipoandikwa Dodoso la Kukusanya Maoni ya Maboresho ya Sheria.,baada ya mchakato wa ukusanyaji maoni kukamilika Tume itatoa taarifa ya na kuanza kufanyia kazi..

Naye Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mstaafu January Msofe aliwataka wajumbe wa baraza hilo wawe huru kuzungumza yote ambayo wanaona kuwa yana manufaa kwa tume hiyo na baraza hilo la wafanyakazi pamoja na Taifa kwa ujumla.