Habari
Profesa Elisante Ole Gabriel Aishauri Tume ya Kurekebisha Sheria Kuhusu Matumizi ya Mifumo ya Kielektroniki
Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel, ameshauri Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) kutumia mifumo ya kielektroniki ili kuweka wazi sheria ambazo zimefanyiwa marekebisho pamoja na manufaa yake kwa jamii.
Akizungumza katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria jijini Dodoma, Profesa Ole Gabriel alisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia katika mchakato wa kurekebisha sheria ni njia bora ya kuongeza uwazi, uwajibikaji, na uelewa wa wananchi kuhusu mabadiliko ya sheria yanayofanywa na tume.
Alieleza kuwa mifumo ya kidijitali inaweza kusaidia Kuhifadhi na kusambaza taarifa za sheria zilizofanyiwa marekebisho kwa urahisi na kutoa fursa kwa wananchi kutoa maoni yao kuhusu mabadiliko ya sheria.
Aidha alisema mifumo itasaidia kuharakisha mchakato wa urekebishaji wa sheria, kwa kuwa mfumo wa kielektroniki unaweza kusaidia kupokea na kuchakata maoni kwa haraka zaidi.
Aidha, alihimiza ushirikiano kati ya Mahakama, Tume ya Kurekebisha Sheria, na wadau wa sheria ili kuhakikisha kuwa sheria zinazorekebishwa zinakidhi mahitaji halisi ya wananchi na kuakisi mabadiliko ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi nchini Tanzania.
Katika maadhimisho hayo, Tume ya Kurekebisha Sheria ilieleza kuwa tayari imeanza kuchukua hatua za kuboresha mifumo yake ya kidijitali, ukiwemo ule wa menejimenti ya taarifa (LRCTIMS) ili wananchi waweze kupata taarifa kwa urahisi zaidi.