Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

PROF. RIZIKI SHEMDOE AFUNGA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA NA KUSISITIZA WATUMISHI WA UMMA KUJITOA KUWAHUDUMIA WANANCHI
24 Jun 2026
PROF. RIZIKI SHEMDOE...

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, amewataka watumishi wa umma kujitoa kikamilifu katika kuwahudumia wananchi, akisema kufanya hivyo kutasaidia kurejesha tabasamu na kuongeza imani ya wananchi kwa huduma za serikali.

Kauli hiyo ameitoa leo, Juni 23, 2026, katika Viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma, alipokuwa akihutubia wakati wa kufunga Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt.Moses Kusiluka.

Alisema watumishi wa umma wana nafasi muhimu katika kuharakisha maendeleo ya taifa kupitia utoaji wa huduma zenye weledi, uadilifu na uwajibikaji kwa wananchi.

Awali Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi alisema baadhi ya malalamiko yanayojitokeza katika taasisi za umma yanachangiwa na wakuu wa taasisi pamoja na maafisa rasilimali watu kushindwa kuwahudumia watumishi kwa wakati.

Mkomi alisema changamoto hiyo inatokana na baadhi ya viongozi kutokuwa tayari kutumia mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika utekelezaji wa majukumu yao, hali inayochelewesha utatuzi wa maombi na huduma mbalimbali zinazowasilishwa na watumishi kupitia mifumo hiyo.

Alieleza kuwa matumizi sahihi ya TEHAMA yanaweza kuongeza ufanisi, uwazi na kasi ya utoaji wa huduma, huku akisisitiza umuhimu wa viongozi kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika utendaji kazi.

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ni miongoni mwa tasisi za serikali iliyoshiriki kikamilifu
Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza Juni 16, 2026 na kuhitimishwa leo Juni 23, ambapo wananchi waliotembelea banda la tume walipata elimu na ushauri kuhusu sheria mbalimbali pamoja na kutoa maoni yao kuhusu mapendekezo ya maboresho ya sheria.