Habari
MAKAMU WA RAIS AITAKA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA NCHINI KUFIKISHA ELIMU YA SHERIA VIJIJINI ILI KUPUNGUZA MIGOGORO YA ARDHI
Makamu wa Rais Dr. Philip Mpango ameagiza Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania kuendelea kutoa elimu ya Sheria kwa wananchi hususan wa maeneo ya vijijini Katika masuala ya migogoro ya umiliki wa ardhi na mirathi ambapo ni miongoni mwa masuala yanayo lalamikiwa na wananchi wengi.
Maelekezo hayo ameyatoa leo wakati alipotembelea banda la elimu ya sheria kwa umma la Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria (Mama Samia Legal Aid) iliyozinduliwa leo Katika uwanja wa Majimaji ulioko Songea, Mkoani Ruvuma.
Dr.Mpango ameeleza pia wananchi wengi wanalalamika kuhusu changamoto wanazozipata Katika suala la umilikishwaji wa ardhi pamoja na mirathi. Hivyo, ni jukumu la Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kuhakikisha kwamba wanawafikia wananchi waliopo vijijini wakati wa kutoa elimu ya sheria kwa umma ili wananchi hao wajue haki na wajibu unaowahusu kisheria.
"Twendeni vijijini kutoa elimu ya sheria na kukusanya maoni na mapendekezo hususan kwenye masuala ya ardhi na mirathi, huko kuna malalamiko mengi ni lazima marekebisho yetu yaendane na changamoto zinazowakabili wananchi." Alisema Mpango.
Aidha Dr. Mpango ameeleza kwamba pamoja na elimu ya Sheria inayotolewa na Tume hiyo bado kuna umuhimu wa matokeo ya tafiti za Tume kuwafikia wananchi hivyo, ameagiza taarifa (ripoti) za tafiti hizo ziandikwe kwa lugha ya kiswahili ili watanzania wengine waweze kuelewa kwa urahisi.
Ameeleza kwamba tafiti nyingi zimekuwa zikifanyika lakini matokeo yake zinaandaliwa kwa lugha ya kingereza hivyo wananchi wengi kushindwa kuelewa.
Pamoja na maelekezo hayo Makamu wa Rais ametoa pongezi kwa Tume ya kurekebisha Sheria pamoja na taasisi nyingine zinazotoa msaada wa kisheria kwa wananchi kwa kusaidia suala la upatikanaji wa haki huku akisisitiza kwamba elimu ya sheria itumike kupunguza migogoro mbalimbali inayojitokeza Katika jamii.
Awali Katibu Mtendaji wa Tume hiyo bwana Griffin Mwakapeje amesema Tume hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzipitia sheria mbalimbali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutoa Mapendekezo ya uboreshaji ambapo ameeleza kwamba itasiadia Sana kuondoa migogoro kwa wananchi na kuongeza nguvu ya kukuza uchumi wa nchi.
Ameendelea kueleza kuwa jukumu jingine la Tume ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa Sheria ili kubaini endapo maelengo ya kutungwa kwa Sheria hizo yamefanikiwa Jambo ambalo ameeleza kwamba Tume inaendelea kulitekeleza kwa Kasi.
Hata hivyo ameeleza wamejipanga kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu maboresho ya Sheria pamoja na mambo mengine ya kisheria ambapo ameeleza kwamba itasaidia kupunguza migogoro mingi Katika jamii inayosabishwa na changamoto za kisheria
Naye bwana Ismail Hatibu Wakili wa Serikali kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania amefafanua kwamba Tayari wameshaanza kuandika taarifa za matokeo ya tafiti zake kwa lugha ya kiswahili ambapo itasaidia wananchi wengi kuzielewa taarifa hizo na kuwafikiwa wananchi walio wengi.
Wakili Hatibu ameeleza kwamba kwa Sasa Tume inatumia vyombo vya habari Kama radio, televisheni, magazeti, mitandao ya kijamii, makongamano, warsha, semina na maonesho mbalimbali kwa lengo la kufikisha elimu kwa wananchi lengo hususan wale walioko mbali.
Vile vile, Tume ipo Katika hatua za mwisho za kukamilisha taarifa ya Mapitio ya Mfumo wa Sheria zinazosimamia Makosa dhidi ya Maadili ambapo taarifa hiyo itawafikia wananchi ikiwa Katika lugha ya kiswahili.