Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

Habari

ELIMU YA SHERIA ITOLEWE KWA KUSULUISHA ISIWE KUMSAKA MSHINDI – NAIBU WAZIRI MKUU MHE, DOTO BITEKO.


Naibu Waziri mkuu na Waziri wa Nishati Mhe, Dkt. Doto Biteko amewataka wataalamu wanaokwenda kutoa huduma ya msaada wa kisheria katika maeneo mbali mbali kuweka nia ya kutafuta suluhu miongoni mwa jamii husika badala yake wasiende kutafuta nani mshindi katika jamii hiyo.

Biteko ameyasema hayo tarehe 26 Mei 2024 katika viwanja vya stendi ya zamani ya mabasi mkoani Njombe wakati akizindua kampeni ya utoaji elimu ya msaada wa kisheria Mama samia Legal Aid Campaign ambapo inategemewa kufanyika kwa muda wa siku kumi kuanza Mei 26 hadi tarehe 4 ya mwezi Juni mwaka huu, huku wataalamu wa masuala ya kisheria wakitegemewa kutembelea kutoa elimu wilaya zote za mkoa huo.

Akikisitiza kuwaasa wataalamu hao wanaokwenda kutoa elimu kwa jamii Biteko aliongeza kusema kuwa kitendo cha Kwenda kuunda upatanishi kwa njia ya kumtafuta mshindi haitakua njia sahihi kwani itazidi kuongeza tatizo la kuundwa visasasi badala yake wataalamu hao wakahakikishe wanawaweka Pamoja na kuwavuta Pamoja wana jamii wanaopitia changamoto mbali mbali za kisheria.

“Lengo lenu la kwanza liwe ni kutafuta suluhu miongoni mwa hiyo jamii badala ya kutafuta nani mshindi, tukienda kutafuta mshindi tutamaliza kutoa nasaha na tutaacha roho za visasi upande wa pili kwa sababu mwanadamu yupo hivo asingependa kushindwa wakati wote” alisema Biteko

Awali akitoa taarifa ya Wizara ya Katiba na Sheria Waziri wa wizara hiyo Balozi Dkt. Pindi chana alisema uendeshwaji wa kampeni hiyo ni uendelezaji misingi ya utawala bora ambayo inasimamiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na kusisitiza wananchi kuendelea kunufaika na huduma hiyo katika kusuluisha changamoto mbali mbali ambayo inatolewa bure bila malipo.

“Sisi sote ni mashuhuda hata Rais anapokua katika ziara zake anasimama kila mahali kuwasikiliza wananchi na sasa ametutuma sisi kusikiliza kero za kisheria kwa wananchi na kuwasaidia kutatua kwakweli tunamshukuru sana Rais kwa kuhimarisha Utawala bora” alisema Balozi pindi Chana.

Kwa upande wake katibu Mtendaji wa Tume ya kurekebisha sheria Tanzania, George Mandepo alisema kampeni hiyo imezidi kutoa nafasi kwa Tume hiyo kuendelea kutoa elimu ya kisheria kwa Umma na kubainisha kuwa mategemeo ni makubwa ya wananchi kufika katika Banda la tume lililopo stendi ya zamani ya mabasi ambapo kampeni hiyo pia inaedelea ili kutoa elimu ya kisheria juu ya masuala mbali mbali.

“Tunaona kuwa ni faida kubwa kwa wananchi hasa ikizingatiwa huduma hii inawafikia wananchi wala haaiitaji malipo yeyote, sisi kama Tume ya kurekebisha sheria tunawakaribisha wananchi wafike kupata elimu ya kisheria ili iweze kuwasaidia kutatua changamoto zao zinazohusiana na masuala ya kisheria”. Alisema Mandepo.