Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

Habari

WAZIRI DKT.NDUMBARO ATOA MAELEKEZO TUME YA KUREKEBISHA SHERIA TANZANIA, ASISITIZA MAADILI NA UWAJIBIKAJI


Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (Law Reform Commission of Tanzania - LRCT) ni injini ya Sekta ya Sheria nchini ambayo imeundwa na Serikali na kukasimiwa majukumu ya kurekebisha sheria nchini ili kuhakikisha uwepo wa haki na maendeleo ya taifa kwa wananchi ambapo ni vema kutekeleza majukumu kwa kuzingatia maadili, sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma.

Hayo yameelekezwa na Mhe. Dkt Damas Ndumbaro (Mb), Waziri wa Katiba na Sheria wakati akifungua mkutano wa kikao kazi cha mafunzo baina ya viongozi wa Wizara na watumishi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania yaliyofanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 13-15/12/2022 kwenye Ukumbi wa Ofisi za Bunge, Dar es salaam.

Waziri Dkt. Ndumbaro amesema kuwa LRCT ni injini ya kurekebisha sheria nchini hivyo amewataka Watumishi kutambua kuwa wamebahatika kupewa jukumu la kufanya kazi kwenye Tume na amewahimiza kuzingatia maadili, sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma kwa vitendo, kwa kujitoa sadaka na kutumikia cheo alichopewa ili kuwapatia wananchi huduma stahiki.

“ Hii ni taasisi ya umma na siyo ya kwenu binafsi, lazima msimame kwenye sheria, taratibu na kanuni na siyo kutoka nje ya sheria, taratibu na kanuni kwakuwa sisi wote ni watumishi wa umma na hakuna mwenye hati miliki ni muhimu mfanye kazi kwa kuzingatia uzalendo, tuchape kazi kwa bidii, tuheshimu mamlaka ili kuifanya Tume ing’ae, iendelee kuwa na thamani na kukubalika” amesisitiza Mhe. Dkt. Ndumbaro.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi Mary Makondo amesema kuwa viongozi na watumishi wa tume watapatiwa mafunzo kuhusu maadili kwa watumishi wa umma, utawala bora na kutokomeza rushwa katika utumishi wa umma.

Amesema, Lengo la wizara kutoa mafunzo hayo ni kuhakikisha yanawawezesha kutekeleza majukumu yao kisheria kwa ajili ya haki na maendeleo ya taifa ili kuwa na uwajibikaji kwa kuzingatia maadili ya watumishi wa umma na mafunzo hayo yanatolewa na Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, TAKUKURU na Sekretarieti ya viongozi wa maadili ya utumishi wa umma

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Tume, Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Januari Msofe amesema kuwa Tume imezingatia maelekezo ya Waziri Dkt. Ndumbaro hususani masuala ya maadili kwa kuwa maadili ni kila kitu, maadili ni popote iwe nyumbani, kazini na mbele ya jamii hivyo pamoja na mafunzo yaliyotolewa viongozi na watumishi wametambua kuwa ni muhimu kuendelea kujifunza ili kuweza kutekeleza vema majukumu na kuhudumia wananchi.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume, Casmir Kyuki ameishukuru Wizara kwa kuendeleza utaratibu wa kusimamia Tume na anaamini kupitia mafunzo hayo watumishi watatoka na mwamko mpya wa kutekeleza majukumu.