Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

Habari

Watumishi Watakiwa Kuimarisha Mawasiliano na Kuleta Mrejesho


Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Pindi Hazala Chana amezitaka taasisi zote ambazo zipo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria kuimarisha mawasiliano ya ndani na nje pamoja na kuleta mrejesho wa maagizo mbalimbali yanayotolewa na Serikali.

Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 15/04/2024 wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano uliyopo katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kibaha, Mkoani Pwani.

Waziri Dkt. Pindi Chana amesema mawasiliano ni muhimu katika kuendesha Serikali na kuelezea mafanikio ya Serikali kwa wananchi hivyo ni muhimu mawasiliano yakaimarishwa na kusaidia kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa wakati.

Aidha ameagiza watumishi wote waliopo chini ya Wizara hiyo kuhakikisha wanatoa mrejesho wa utekelezaji wa maagizo ya Serikali huku akibainisha kwamba kila jukumu au agizo liwekewe ukomo wa muda utekelezaji (deadline) ili kuongeza tija katika usimamizi wa majukumu.

“Viongozi wanapotoa maagizo kwa watumishi, watumishi hao wanapaswa kuyatekeleza kwa wakati na sio kusubiri mpaka wakumbushwe kuhusu utekelezaji huo. Vile vile wanatakiwa baada ya kutekeleza maagizo hayo kutoa mrejesho wa utekelezaji huo ili kukamilisha msingi mzima wa mawasiliano” Dkt. Pindi Chana.

Hata hivyo Waziri amewaomba watumishi wote kuhakikisha wanatumia haki yao ya Kikatiba kwa kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuchagua viongozi ili kutimiza haki yao ya kikatiba na hivyo kukuza kidemokrasia.

Awali akimkaribisha Waziri huyo, Katibu Mtendaji Tume wa Kurekebisha Sheria Tanzania Bw. George Mandepo ameeleza kuwa katika Mkutano huo mada mbalimbali yatajadiliwa yakiwemo Maboresho ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004; Mabadiliko ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022; Maboresho ya Mifumo ya TEHAMA na Umuhimu wake katika Uendeshaji wa Shughuli za Serikali; na Mwenendo wa Maboresho ya Muundo wa Tume ya Kurekebisha Sheria.

Aidha, Katibu Mtendaji Bw. Mandepo ameeleza kwamba Tume imeweza kutekeleza majukumu mbalimbali kama yalivyopangwa katika Mpango na Bajeti wa mwaka 2023/2024 ikiwa ni pamoja na kukamilisha Taarifa ya Utafiti wa Mfumo wa Sheria Unaosimamia Makosa Dhidi ya Maadili. Tume inaendelea kutekeleza Mpango na Bajeti wa mwaka 2023/2024 kwa kukamilisha Taarifa za Mapitio ya Mfumo wa Sheria Unaosimamia Dhamana, Taarifa ya Mapitio ya Adhabu ya Viboko, Taarifa ya Tathmini ya Utekelezaji wa Sheria za Sekta ya Usafiri Ardhini, Taarifa ya Tathmini ya Utekelezaji wa Sheria Zinazosimamia Hakimilki na Hakishiriki, na Taarifa ya Utafiti wa Mfumo wa Sheria Unaosimamia Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa alieleza Katibu mtendaji huyo.

MWISHO