Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

Habari

UHALIFU HAULIPI JAMII IJITAHIDI KUJITAFUTIA KIPATO CHA HALALI


Hayo yameelezwa na Naibu katibu wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bi. Zainab Chanzi alipokua anazungumza katika Redio Mpanda Fm kupitia kipindi cha “kumekucha Tanzania” kilichoruka Novemba 4 mwaka 2024 Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi, ambapo mada kuu ilikua ikileza elimu ya sheria juu yatokanayo na uhalifu.

Akitoa rai kwa wananchi kupitia Redio hiyo Zainab alisema ni vyema wananchi wakaelewa kuwa uhalifu haulipi na iwapo ukajipatia mali kinyume na sheria mali hiyo itataifishwa Kwenda Serikalini au kurudishwa kwa muathiriwa wa kitendo hiko cha uhalifu Pamoja na adhabu nyingine kama kulipa faini na kifungo gerezani.

“Mimi nashauri wana Jamii tufuate sheria, tufanye kazi za halali na tutape vipato kwa njia halali hakutakua na mtu atakaekuingilia ukiwa na kipato cha halali” alisema Zainab.

Hata hivyo Zainab alisema pamoja na majukumu mengine ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania alieleza Tume hiyo kuwa inatoa elimu ya sheria kwa Umma ili kuwafanya wananchi kuwa na uwezo wa kuitekeleza sheria bila shuruti.

Awali afisa sheria Jackline Nungu alisema mapato yatokanoyo na uhalifu ni mali, fedha au faida ambayo inapatikana baada ya mtu kutenda uhalifu akitolea mfano wa usafirishaji wa wahamiaji haramu ambao wanaoingia nchini kinyume cha sheria ili kujipatia fedha.

“Sheria haitaruhusu mtu afaidike kutokana na uhalifu wala kutumia fedha hizo kufanya uhalifu mwingine kama kufadhili shughuli za ugaidi” alisema Jackline.

Jackline aliendelea kueleza kuwa hata matukio ya unyang’anyi, wizi na uporaji ambayo yanazalisha kipato kwa mtenda tukio pia ni sehemu ya mapato yatakonayo na uhalifu kwa kuwa mali husika zimepatikana katika namna ya uhalifu.

Akifafanua kuhusu Sheria zinazosimamia Mapato yatokanayo na uhalifu Jackline alisema suala hilo ni mtambuka linaloguza Sheria nyingi ikiwemo: Sheria ya mapato yatokanayo na Uhalifu, Sheria ya udhibiti wa makosa ya uhujumu Uchumi na uhalifu wa kupangwa, Sheria ya mwenendo wa makosa ya Jinai, Sheria ya kuzuwia na kupambana na Rushwa,Sheria ya Kuzuwia na kudhibiti Dawa za kulevya na Sheria ya kuzuwia Usafirishaji haramu wa Bianadamu

“Sababu sheria inasema mtu hatakiwi kufaidika na uhalifu” alisisitiza Jackline.

Aidha afisa sheria Jackline alisisitiza pia kuwa Jamii inapaswa kuwa mbali na uhalifu kwakua sheria zilizotungwa zinalenga kuwawajibisha watakaokiuka huku akihimiza wananchi kuendelea kupokea elimu ya sheria kwa kuwa kutojua sheria sio kinga utawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeendelea na utoaji wa elimu ya sheria kwa Umma kupitia vituo vya Redio ili kuongeza uelewa kwa wananchi kuishi kwa kutii sheria bila shuruti.