Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

Habari

TUMESHERIA YASHIRIKI MAONESHO YA NNE YA SIDO MKOANI NJOMBE


TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) imeshiriki Katika maonesho ya Nne ya SIDO yaliyofanyika Katika uwanja wa Saba saba Mkoani Njombe na kutoa elimu ya Sheria kwa wajasiriamali mbalimbali walioshiriki maonesho hayo.

Wakiwa Katika maonesho hayo Tume hiyo ilikutana na wajasiriamali mbalimbali wakiwemo waganga wa tiba mbadala ambapo walipata elimu juu ya Sheria ya Tiba za asili na Tiba mbadala namba 23 ya mwaka 2002.

Akitoa elimu kwa wajasiriamali hao Wakili wa Serikali Ismail Hatibu amewataka wajasiriamali hao kufuata matakwa wa Sheria hiyo ikiwemo kujisajili na kuhakikisha dawa hizo zinalinda Afya na zinakuwa na manufaa kwa wananchi.

"Sheria ya Tiba za asili na Tiba Mbadala namba 23 ya mwaka 2002 inamtaka kila Mganga wa tiba mbadala kujisajili Katika mabaraza husika ikiwa ni pamoja na kitambulisha aina za huduma anazozitoa, ni vyema kuhakikisha Sheria inafuatwa kwa manufaa ya nchi na wananchi kwa ujumla"alisema Hatibu.

Kwa upande wa wajasiriamali hao walitoa Maoni Yao kuhusu uboreshaji wa Sheria hiyo ili kufikia lengo kusudiwa na kupatikana kwa gharama nafuu.

Akiongea wakati wa mahojiano mjasiriamali Tamji Amiri wa Tambi Harbal Product alieleza kwamba Bei ya dawa hizo zimekuwa za juu kwa kuwa gharama ya usajili ni kubwa Jambo ambalo ameeleza kwamba mbali ya kuchukua muda mrefu lakini kunafanya waganga wengi kushindwa kusaiji dawa zao.

Hata hivyo ameiomba Serikali kupitia Tume hiyo kuzifanyia maboresho Sheria hiyo ili wadau waweze kusajili dawa zao kwa urahisi kupitia mabaraza yaliopo kuliko Sasa ambapo usajili mpaka kumfikia mkemia Mkuu wa Serikali inachukua muda mrefu na gharama inakuwa kubwa.

Naye Hashimu Kaseke kutoka kampuni ya Kaseke Herbal product amesema wamekuwa wakipata changamoto kubwa ya upatikanaji wa vibali hasa wanapokwenda Wilayani Jambo ambalo limekuwa likikwamisha uuzaji wa dawa maeneo mbalimbali ya nchi.

Aidha bwana Kaseke ameiomba Serikali kuchukua tahadhari kwa dawa ambazo zinasajiliwa kutoka nje ya nchi huku za kwao zikiwekewa vikwazo vingi Katika usajili Jambo ambalo linaweza kupunguza ushindani wa Biashara hizo.

Maonesho hayo yamefunguliwa rasmi tarehe 24/10/2023 na Naibu wa Waziri wa uwekezaji viwanda na Biashara Mhe.Exaud Kigahe, ambapo alisisitiza umuhimu wa wajasiriamali kufuata taratibu na kanuni ili kazi yao iwe chanzo cha ukuaji wa uchumi wa Taifa.