Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

Habari

TUMESHERIA YAINGIA DARASANI KUTOA ELIMU YA SHERIA


TUME ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) imeanza kutoa elimu kuhusu sheria mbalimbali katika shule za msingi na sekondari za Mkoa wa Rukwa kwa lengo la kuongeza uelewa wa sheria na utii wa sheria bila shuruti.

Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Sheria kwa Umma ambaye pia ni Naibu Katibu Mtendaji, Zainabu Chanzi, alisema miongoni mwa majukumu ya Tume hiyo ni kutoa elimu kwa umma ili kuisaidia jamii kuzielewa sheria na hivyo kupunguza utendekaji wa makosa mbalimbali ya jinai.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana, Chanzi alisema elimu hiyo itakayotolewa kwa siku mbili katika shule za Manispaa ya Sumbawanga ni kuhusu Sheria ya Mtoto,Makosa dhidi ya Maadili ya Utu,Makosa ya Kimtandao, Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa, Gerald Kusaya ameipongeza Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) kwa uamuzi wake wa kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi.

Kusaya alisema zoezi hilo litakuwa na tija kubwa kwani jamii ina uhitaji mkubwa wa elimu ya sheria na kwamba elimu hiyo itawasaidia watoto kufahamu haki na wajibu wao na kujiepusha kutenda makosa mbalimbali yaliyoanishwa katika sheria husika.

" Niwapongeze kwa uamuzi wa kutembelea wanafunzi na kuwapa elimu ili watambue haki na wajibu wao katika jamii, kwa kweli huduma yenu inahitajika sana Mkoani hapa" alisema.

Aidha, Katibu Tawala huyo ameiomba Tume hiyo kuendelea kutoa elimu hiyo kwenye shule na vikundi mbalimbali vya vijana na wajasiriamali kwa kuwa uelewa wa sheria utasaidia wananchi kutii sheria bila shuruti.

Kusaya alishauri elimu hiyo kuendelea kutolewa katika makundi mbalimbali ya jamii bila kusuburi watende makosa na kufikishwa mahakamani.