Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

Habari

TUME ZA KUREKEBISHA SHERIA TANZANIA NA ZANZIBAR ZIMESAINI MKATABA WA USHIRIKIANO


TUME za Kurekebisha Sheria Tanzania na Zanzibar zimesaini mkataba wa maeneo ya kushirikiana utakaowawezesha kushughulikia changamoto za kisheria zinazojitokeza katika nyanja mbali mbali kama vile uchumi, Ulinzi, haki za binadamu na mazingira

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini ushirikiano huo Julai 12,203 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Jaji mstaafu, January Msoffe amesema kuwa ushirikiano huo pia utawezesha kushughulikia masuala muhimu ya kisheria ambayo yanahitaji juhudi za pamoja.

"Ushirikiano huu ni hatua madhubuti ya kuimarisha mifumo ya sheria na kuboresha maisha ya watanzania kwa kuimarisha ubora wa upatikanaji na ufikiwaji wa sheria hizo" amesema Msoffe

Aidha Jaji Msoffe amesema kupitia ushirikiano wao wataweka mazingira wezeshi kwa ukuaji wa uchumi, uwekezaji na umoja na mshikamano ndani ya kijamii hivyo, wanaamini mfumo thabiti wa kisasa wa kisheria ndio msingi wa jamii yenye haki na ustawi.

Alisema kuwa ushirikiano kati ya tume hizo unathibitisha kuimarisha mfumo wa kisheria unaozingatia utawala bora na utawala wa sheria kwa maendeleo ya jamii.

"Ushirikiano huu utakuwa jukwaa muhimu la kubadilishana ujuzi, utaalamu na mbinu bora katika nyanja ya mageuzi ya sheria katika nchi, tutatumia nguvu zetu ili kuimarisha utafiti wa kisheria, mapitio na tathmini ya sheria zilizopo na kubainisha maeneo mbalimbali yenye changamoto na kujitahidi kuondoa upungufu au mapengo yanayoweza kuwepo kati ya mifumo ya sheria. "Amesema Jaji Msoffe.

Naye, Khadija Shamte Mzee, Mwenyekiti wa tume hiyo amesema kuwa bado umuhimu wa tume hizo haujaonekana katika jamii hivyo wanapaswa kubadilisha mtazamo.

Mzee amesema mpaka sasa wao kama Tume wanaonekana mzigo katika utekelezaji wa majukumu yao hivyo kwa kushirikiana watahakikisha wanafanya mabadiliko na kupunguza gharama ili kutimiza matakwa ya serikali.

Ameongeza kuwa ni wakati wa kuongeza kasi ya utendaji kazi wao wa kufanya mapitio ya sheria, kubadilisha na kutafiti zitumike kwenye jamii na serikali ione huduma zao.

Akielezea mkataba huo, Katibu Mtendaji wa tume Zanzibar, Mussa Kombo Bakari amesema mkataba huo una maeneo 10 ambayo ni kuimarisha ushirikiano baina ya tume hizo.

Pia kubadilishana taarifa ikiwemo ripoti za utafiti na nyaraka, kufanya tafiti za pamoja, kubadilishana utaalamu na uzoefu baina ya pande zote.

"Mkataba huu utaongeza utaalamu katika uandishi wa sheria na miswada. Itaundwa timu ya kuratibu na kutekeleza hati hii na kushauri, kuhakikisha usiri na mawasiliano," alisema Bakari.

Awali akieleza majukumu ya tume hizo Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Griffin Mwakapeje amesema Kazi ya tume hizo ni kufanya mapitio ya Sheria zote za Tanzania na Zanzibar ili ziweze kuendana na Mazingira na jamii iliyopo.

Hata hivyo ameendelea kusema kwamba zipo sheria ambazo zinatakiwa kuondolewa na kwa kuwa zimekuwa za zamani na zipo ambazo zinatakiwa kusasishwa na na kufanya mapendekezo ya kutungwa Sheria nyingi kulingana Mazingira yaliyopo.