Habari
SI HIARI TENA KUTOA HUDUMA KWA NJIA YA MTANDAO – WAZIRI SIMBACHAWENE
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora Mhe, George B. Simbachawene alisema ni lazima kwa Tasisi za Umma kuingia na kutoa huduma kupitia mifumo na kwamba si hiari kwakua matumizi ya mifumo husaidia kuepusha mazingira ya rushwa katika kutenda haki kwa wanaohudumiwa.
Mhe, Simbachawene aliyasema hayo tarehe 6 Februari 2024 katika ukumbi wa AICC mkoani Arusha alipokua akifungua kikao kazi cha 4 cha Serikali Mtandao (eGA) kilichohudhuriwa na Maafisa mbali mbali wa Serikali kutoka katika Taasisi, Mashirika ya Umma.
“Kwa Taasisi za Umma ndio kabisa ni lazima kuingia katika mifumo kwa sababu kwa kufanya hivo ndipo tutaondosha hata malalamiko ya wananchi wanaohitaji huduma” alisema Mhe, Simbachawene
Kwa upande wake Mkurugenzi rasilimali watu na Utawala Tume ya kurekebisha sheria Tanzania (LRCT) Bw. Mohamed Mavura alisema kutokana na umuhimu wa kukua kwa teknolojia ni Vigumu kutofautisha Tehama katika kutekeleza majukumu ya Tume hiyo kwakua miongoni mwa majukumu ya Tume ni pamoja na kuchukua maoni ya wananchi ambao hutumia Teknolojia ya Tehama katika kuwasilisha maoni yao.
“Kimsingi hatuwezi kutofautisha Tehama na Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kwakua inapokea maoni ya wananchi ambao wengi wao hutumia tehama kuyawasilisha” Alisema Mavura
Kikao kazi cha 4 cha serikali Mtandao (eGA) kinachoendelea mkoani Arusha kinategemewa kufanyika tarehe 6-8 Februari 2024 huku mambo mbali mbali yaUtoaji huduma kwa kutumia mifumo yakitegemewa kujadiliwa.