Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

Habari

SERIKALI KUANZISHA TUME YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI KATIKA MIFUMO YA TEHAMA.


Mkurugenzi kitengo cha Usalama na Mawasiliano ya Teknolojia ya Habari Mhandisi Stephen M. Wangwe alisema Serikali imeanzisha Tume ya Ulinzi wa Taaarifa binafsi katika matumizi ya mfumo wa TEHAMA na imeandaa Mwongozo wa matumizi bora, sahihi na salama ikiwemo Ulinzi na usalama wa taarifa binafsi,Mifumo vifaa na Miundombinu ya TEHAMA.


Wangwe ameyasema hayo alipokuwa anawasilisha Mada ya Sera ya Taifa ya TEHAMA tarehe 7 Februari 2024 wakati wa kikao kazi cha 4 cha Serikali Mtandao kinachoendelea katika ukumbi wa AICC Mkoani Arusha na kueleza kuwa malengo ya sera hiyo ni kukuza mazingira ya kidijitali ya kina, salama na jumuishi ikihusisha Ulinzi na usalama katika mifumo ya kidijitali Pamoja na Ulinzi na usalama Mtandaoni.


“Jitihada zinazofanyika mpaka sasa ni uhuishaji wa mkakati wa usalama wa mtandao 2024-2029 ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia sambamba na uanzishwaji wa Tume ya Ulinzi wa taarifa binafsi” alisema Wangwe

Aidha katika hatua hiyo Afisa TEHAMA wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) Bw. Selemani Shabani alisema kuanzishwa kwa Tume ya ulinzi wa taarifa binafsi kutaongeza ufanisi kwakua itasaidia kuzuwia taarifa kutokuwafikia watu wasiolengwa na taarifa husika na badala yake maadili na usiri wa taarifa utaimarika katika Ofisi za Serikali.


Bw. Selemani ameongeza kuwa kwakua tovuti zote za serikali zinasanifiwa, kutengenezwa na kuendeshwa na Mamlaka ya Serikali mtandao (eGA) hivyo jitihada za uimarishaji ulinzi katika mifumo hiyo zitaleta ufanisi na hata kuzuia uhalifu na udukuzi wa nyaraka za Serikali.


“Binafsi naona ni kitu kizuri hasa ukizingatia siku hizi kazi zote ofisini ni Kidijitali kuanza barua pepe za ndani ya Tume na hata kutuma katika Wizara na Taasisi zingine, muhimu sana kuimarishwa kwa usalama wa matumizi katika mawasiliano tunayotumia kila siku” alisema Bw. Selemani

Sheria ya ulinzi ya taarifa Binafsi ya mwaka 2022, kanuni (2) na miongozo minne (4) mifumo ya usajili na ushughulikiwaji wa malalamiko imekamilika ili kuanza kutekelezwa katika kushughulikia ulinzi wa taarifa binafsi katika Mifumo ya TEHAMA.