Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

Habari

​Naibu Katibu Mkuu Dr.Khatibu Kazungu afungua kikao cha watumishi Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, awataka kujifunza ujasiriamali.



Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dr.Khatibu Kazungu amewataka wafanyakazi kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wabadilike kulingana na mazingira yaliopo na kuwekeza katika stadi za nje ya mshahara.

Naibu Katibu Mkuu ameyasema hayo leo tarehe 17/04/2024 wakati akifungua mkutano wa wafanyakazi wa Tume ya Kurkebisha Sheria Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Uongozi Mwl. Julius Kambarage Nyerere iliopo Kibaha Mkoani Pwani.

Dr. Hatibu Kazungu ameeleza kwamba watumishi wa serikali wanatakiwa kufanya ujasiriamali ili kupata kipato nje ya mshahara wa utumishi ili kuondoa changamoto zinazojitokeza wakati wa kustaafu.

Aidha, amewataka watumishi hao kufuatilia kwa makini mafunzo ya ujasiriamali mada itakayotolewa na Dr. Deo Sabokwingina, Mkurugenzi wa kituo cha ujasiriamali na ubunifu kutoka chuo kikuu cha Iringa katika mkutano huo ili kuwaongezea ujuzi na nafasi mbalimbali katika maisha.

“Mtumishi anatakiwa kujipanga kustaafu siku alipopata ajira, kwa wale ambao hawajajipanga bado hawajachelewa nimeona mtaalamu wa mambo ya ujasiriamali amepangiwa kutoa mada ya ujasiriamali tumieni fursa hii kujifunza kutafuta fedha nje ya mshahara ” Alisema Hatibu Kazungu.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Bw. George Mandepo amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa muda wa siku mbili na mada zitakazo tolewa ni uzalendo na utaifa itakayotolewa na Bw. Philip Mangula Makamu Mwenyekiti mstaafu chama cha mapinduzi, utumishi na utawala itakayotolewa na Dkt. Francis Michael kutoka shule ya uongozi ya Mwalimu Nyerere, muundo wa serikali , ujasiriamali na mada ya kukubali mabadiliko itakayotolewa na Dr.Chris Mauki kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Mandepo aliendelea kueleza kwamba mada nyingine zitakazotolewa ni namna ya kukabiliana na changampoto ya afya ya akili, Itifaki ushirikiano kazini na usalama wa serikali na matumizi sahihi na salama ya kumbukumbu na nyaraka katika serikali itakayotolewa na Msuya Natihaika hivyo kuwataka watumishi kuzingatia mafunzo hayo ili yawe chachu katika maisha yao ya kazini na wakiwa nje ya kazi.