Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

Habari

MKUTANO WA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA TANZANIA (LRCT) NA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA ZANZIBAR KULETA MATOKEO CHANYA.Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) na Tume ya Kurekebisha Sheria ya Zanzibar leo tarehe 11/03/2024 zimekutana katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar kwa lengo la kujadiliana namna ya kuimarisha ushirikiano wao katika kazi za mapitio na utafiti wa sheria mbalimbali za Muungano hasa zinazosimamia mambo ya maadili ili kupunguza kadhia ya ukosefu wa maadili katika jamii

Akiongea katika kikao kazi hicho Katibu Mtendaji Tume ya Kurekebisha Sheria Bw. George Mandepo alisema kikao hicho kinalenga kuimarisha uhusiano baina yaokatika utafiti na mapitio ya sheria na kimelenga kuongeza wigo wa kufanya mapitio ya sheria zinazosimamia maadili.

Aidha Mandepo ameeleza kwamba katika kikao hicho wameadhimia uwepo wa mafunzo ya pamoja ya ndani na nje ya nchi kama sehemu ya kuwajengea uwezo watumishi wa Tume hizo ikilinganishwa na hali ilivyo sasa ambapo kila upande ulikuwa na utaratibu wa tofauti wa kuwajengea uwezo watumishi.

“ tumekubaliana mambo mengi ya msingi moja wapo ikiwa ni kuandaa na kushiriki mafunzo ya pamoja ya ndani na nje ya nchi kwa watumishi wetu ili kuwajengea uwezo” alieleza Mandepo.

Aidha Bw. Mandepo ameeleza umuhimu wa kutumia mifumo ya TEHAMA katika kuweka na kusambaza taarifa muhimu za Tume hizo ili kuwafikia wadau wengi kwa wakati huku akibainisha kwamba wamekubaliana kufanya vikao vya mara kwa mara ambavyo vitasaidia kuongeza ufanisi.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar Bw. Musa Kombo Bakari akitoa shukrani zake ameishukuru LRCT ambapo ameeleza kwamba kikao hicho kimetoa mwanga hasa katika kipindi hiki ambacho wanaendelea na mapitio ya sheria zinazosimamia mambo ya maadili ambapo kwa Tanzania bara walikuwa wameshapiga hatua katika ukamilishaji wa kazi hiyo.

Hata Hivyo Bw. Kombo ameendelea kueleza umuhimu wa mashirikiano hayo ambayo yatasaidia kubadilishanauzoefu wa kazi na kupata mawazo mapya hasa wakati huu ambao wapo katika hatua mbalimbali za kutafsiri sheria kwa lugha ya Kiswahili.

“kukutana kwetu leo kumetuongezea kitu,hili linadhihirisha kwamba tutakavyokuwa tunakutana kutasaidia kupata mawazo mapya ambayo yatakuwa ni chachu kwenye kazi zetu” Kombo alimalizia.

mwisho