Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

Habari

Mabaraza ya wafanyakazi yatumike Kujenga Demokrasia sehemu za kazi - Kabudi


Mabaraza ya wafanyakazi yatumike Kujenga Demokrasia sehemu za kazi - Kabudi

Mabaraza ya wafanyakazi yanapaswa kutumika kama chombo muhimu katika kuboresha na kuimarisha demokrasia kwenye eneo la kazi badala ya kutumika pekee kukusanya na kupitia maoni ya watumishi .

Kauli hiyo imetolewa tarehe 14/11/2024 na Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Midland iliyopo mjini Dodoma wakati akifungua kikao cha 21 cha baraza la wafanyakazi la Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ambapo ameleleza mabaraza hayo yanahusisha ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maamuzi ya Taasisi au shirika wanamofanyia kazi jambo ambalo huongeza uwazi na uwajibikaji.

Waziri Kabudi ameipongeza Manejimenti ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kwa kutimiza takwa la kisheria la kufanya kikao cha baraza huku akifafanua kwamba Baraza la Wafanyakazi halipaswi kuwa chombo cha kupokea malalamiko ya watumishi pekee ingawa ni muhimu kwa baraza hilo kushughulikia malalamiko na changamoto zinazowakabili wafanyakazi na badala yake jukumu lake linapaswa kuwa pana zaidi.

Prof amefafanua kwamba Baraza linaweza na linapaswa kuwa jukwaa la kuchochea maendeleo, kutoa maoni, na kutoa mawazo ya kuboresha ufanisi wa Taasisi kwa ujumla.

Demokrasia katika eneo la kazi ni muhimu kwani inachochea ari ya kazi, kuimarisha ufanisi, na kujenga mazingira yenye amani na haki, alisistiza Waziri wa Kabudi.

“ Baraza la Wafanyakazi si tu chombo cha kusimamia haki za wafanyakazi, bali pia ni nyenzo muhimu ya kufanikisha malengo ya taasisi kupitia ushirikiano wa kweli na mawasiliano ya wazi” alisema Waziri

Amesema Baraza linatoa nafasi kwa wafanyakazi kutoa maoni, mawazo, na mapendekezo kuhusu masuala yanayohusu ustawi wao na maendeleo ya Taasisi kwa ujumla hivyo kupitia Baraza la Wafanyakazi, viongozi watakiwa kupata mawazo mapya ya kuboresha mazingira ya kazi.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Bw. George Mandepo, alieleza kwamba kikao hicho ni hitaji la kisheria na ni muhimu kwa kuwa linashirikisha wafanyakazi katika michakato ya kufanya maamuzi ili kuimarisha ufanisi wa kazi.

Aidha amefafanua kwamba Tume inatekeleza mipango mbalimbali ya kuhakikisha kwamba watumishi wanapata mafunzo ili kuwajengea uwezo na kuboresha ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.

Mkutano huo uliwaleta pamoja wafanyakazi wa Tume na wadau wengine muhimu kwa lengo la kujadili masuala ya kazi, kubadilishana mawazo, na kutafuta suluhisho la changamoto zinazokabili sekta ya sheria.

MWISHO