Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Juma Zuberi Homera ameipongeza Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRC) kwa kufanya kazi kwa weledi na kuendelea kutoa mchango mkubwa katika maboresho ya mfumo wa sheria nchini.
Waziri alitoa pongezi hizo leo tareh 26.11.2025 jijini Dodoma wakati wa ziara yake katika ofisi za Tume hiyo iliyoko Chuo Kiukuu cha Dodoma (UDOM), ambako alipokea taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo pamoja na hatua zilizofikiwa katika mapitio ya sheria mbalimbali.
“Nawapongeza kwa kazi kubwa mnayoendelea kufanya. Mmekuwa mstari wa mbele kuhakikisha sheria zetu zinaendana na mahitaji ya wakati huu, na hilo ni jukumu muhimu kwa maendeleo ya taifa,” alisema Mhe. Waziri.
Alisisitiza kuwa Tume ni mhimili muhimu katika mchakato wa utungaji na marekebisho ya sheria, na kwamba Serikali itaendelea kuisaidia ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Hata hivyo Mhe.Waziri ameishauri Tume kuandaa mpango wa muda mrefu, wa kati na mfupi ili kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake na kuongeza ufanisi katika mchakato wa maboresho ya sheria nchini.
Amesema kuwa mpango wa aina hizo utasaidia tume kupanga kazi zake kwa utaratibu, kuweka vipaumbele vyenye matokeo chanya, na kuhakikisha kuwa marekebisho ya sheria yanafanyika kwa wakati na kwa kuzingatia mahitaji ya taifa.
“Nashauri tume muwe na mpango wa muda mrefu, wa kati na mfupi unaoonyesha ni sheria zipi zinapewa kipaumbele, ni lini zinapitiwa, na ni rasilimali gani zinahitajika. Hii itasaidia kuongeza uwazi, ufuatiliaji na ufanisi katika kazi zenu,” alisema Waziri.
Waziri aliongeza kuwa dunia inabadilika kwa kasi na hivyo ni muhimu kwa sheria za nchi kuhuishwa mara kwa mara ili ziendane na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia. Alisisitiza kuwa mipango imara ya kimkakati itaiwezesha Tume kuendana na kasi hiyo bila changamoto zisizokuwa za lazima.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Winifrida Korosso aliipokea ushauri huo na kueleza kuwa Tume imekuwa ikiandaa mipango ya kazi ya kila mwaka, lakini itaweka mkazo zaidi katika kubuni mpango mpana wa kitaasisi utakaolenga kipindi kirefu na kueleza kwa uwazi mikakati ya maboresho ya sheria nchini.
“Ushauri wa Mheshimiwa Waziri ni muhimu sana. Tutaufanyia kazi ili kuhakikisha tume inakuwa na dira na mikakati thabiti ya muda mfupi, wa kati na mrefu, inayoweza kupimika na kuonyesha matokeo,” alisema Mwenyekiti.
Katika ziara hiyo, Waziri pia alipokea taarifa kuhusu mafanikio, changamoto na miradi inayotekelezwa na Tume, huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kuipa tume ushirikiano na rasilimali muhimu ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Aidha, Mhe. Waziri alisisitiza kwamba tume ianishe sheria zote zilizopitwa na wakati kwa kila wizara na taasis ili ili kuzifanyia mapitio au utafiti ili ziweze kuwa na manufaa kwa watumiaji.
Katika kikao hicho, Waziri aliihakikishia Tume kuwa changamoto hizo zitafanyiwa kazi, akiongeza kuwa wizara yake ina dhamira ya kuimarisha taasisi zote zilizo chini yake ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa haki na ufanisi wa mfumo wa sheria nchini.
“Serikali inatambua umuhimu wa Tume hii. Tutahakikisha mnaendelea kufanya kazi yenu kwa mazingira bora na kwa msaada mnaohitaji,” aliongeza.
Mhe. Alihitimisha ziara yake kwa kuwahimiza watumishi kuendelea kufanya kazi kwa nidhamu, ubunifu na uadilifu ili kuleta maendeleo kwa jamii.