Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Athman Katimba, amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana imani kubwa na kazi inayofanywa na Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRC), kutokana na mchango wake muhimu katika kuhuisha na kuboresha mfumo wa sheria nchini.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kikao kazi na uongozi wa Tume, Naibu Waziri Katimba alisema kuwa Serikali imetambua kwa muda mrefu umuhimu wa tume hiyo, hususan katika kuhakikisha sheria za nchi zinakwenda sambamba na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na teknolojia.
“Rais anaamini katika kazi mnayofanya. Anaiona Tume hii kama mhimili muhimu katika kuhakikisha taifa linakuwa na sheria makini, za kisasa na zinazolinda maslahi ya wananchi. Ninyi ni sehemu ya mabadiliko ya kisheria tunayoyahitaji kama nchi,” alisema Katimba.
Naibu Waziri aliongeza kuwa Serikali itaendelea kuiunga mkono Tume hiyo kwa kuimarisha mazingira ya kazi, kuwajengea uwezo watumishi na kuongeza rasilimali muhimu ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi.
Alisema kuwa Rais amekuwa mstari wa mbele kusisitiza umuhimu wa taasisi zinazohusika na masuala ya kisheria kufanya kazi kwa weledi, uwazi na kasi inayokidhi matarajio ya wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume Jaji wa mahakama ya Rufani Mhe. Winifrida Korosso alimshukuru Naibu Waziri kwa ujumbe huo wa faraja na kubainisha kwamba pongezi na imani hiyo ni motisha kwa Tume kuendelea kufanya kazi kwa bidii na ubunifu.
Katika mazungumzo hayo, Tume iliwasilisha taarifa ya mafanikio yake pamoja na changamoto zinazokwamisha kasi ya mapitio ya sheria, ikiwemo upungufu wa bajeti ya utafiti.
Naibu Waziri aliihakikishia Tume kwamba Serikali itaendelea kushughulikia changamoto hizo, na kusisitiza umuhimu wa kuharakisha marekebisho ya sheria zinazohitajika ili kukidhi mahitaji ya Taifa.