Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Bi. Zainab Chanzi, amesema Tume imeanza rasmi kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia maboresho ya mfumo wa sheria ili kuhakikisha unakidhi mahitaji ya maendeleo ya sasa na ya baadaye ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa maonesho ya sabsaba anayoendelea jijini Dar es Salaam, Bi. Chanzi alisema kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kujenga Tanzania yenye uchumi imara, maendeleo jumuishi na ustawi wa wananchi, hivyo sheria zinapaswa kuendana na mwelekeo huo kwa kuweka mazingira wezeshi ya maendeleo.
Alieleza kuwa Tume imejipanga kufanya mapitio, tafiti na tathmini ya sheria mbalimbali ili kuondoa sheria zilizopitwa na wakati na kuandaa mapendekezo ya maboresho yanayozingatia maendeleo ya sayansi, teknolojia, biashara, uwekezaji na mahitaji ya jamii.
Bi. Chanzi alisema kuwa miongoni mwa maeneo yatakayopatiwa kipaumbele ni sheria zinazohusu sekta za kilimo, uwekezaji, biashara, nishati pamoja na matumizi ya teknolojia mpya kama Akili Unde (AI), ili kuhakikisha zinachangia kikamilifu utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.
Aidha, alisisitiza kuwa Tume itaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu maboresho ya sheria na kushirikisha wadau mbalimbali katika mchakato wa mapitio ya sheria ili kuhakikisha mfumo wa sheria unakuwa shirikishi, wa kisasa na unaochochea maendeleo endelevu.
"Sheria tunazotunga leo ndizo zitakazojenga Tanzania ya baadaye. Hivyo, jukumu letu ni kuhakikisha msingi wa kisheria unawekwa kwa weledi, umakini na kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050," alisema Bi. Chanzi.