Maboresho ya sheria yanayoendelea kufanywa na Serikali yanatarajiwa kuwa msingi muhimu wa mageuzi makubwa katika utawala, uchumi na upatikanaji wa haki, huku yakiweka mazingira bora ya kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza hivi karibuni kuhusu umuhimu wa maboresho hayo, Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Bw. George Mandepo ameeleza kuwa, ilielekezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo mwezi Julai 2025, kuitaka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kushirikiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kufanya maboresho ya kina ya Sheria zote zinazoweza kuleta vikwanzo kwenye kufanikisha malengo ya Dira 2050.
Alibainisha kuwa lengo kuu la maboresho ya sheria ambayo yamekwisha anza chini ya Uratibu wa Tume hiyo kwa ushirikiano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wadau wote wa kisekta kwenye sekta ya umma na binafsi ni kuliwezesha Taifa kuwa na mifumo wa sheria inaoendana na mahitaji ya wakati, kasi ya maendeleo ya teknolojia pamoja na mabadiliko yanayoendelea katika nyanja za kijamii na kiuchumi duniani.
Alisema maboresho hayo ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha sheria zinakuwa nyenzo ya kuchochea maendeleo, kuimarisha utawala bora na kuwezesha mazingira rafiki kwa uwekezaji na ubunifu.
“Sheria bora na madhubuti ni msingi wa maendeleo endelevu. Maboresho haya yanalenga kuhakikisha mfumo wetu wa kisheria unaendana na mahitaji ya sasa na matarajio ya taifa kuelekea mwaka 2050,” alisema Bw. Mandepo.
Alieleza kuwa moja ya manufaa makubwa ya maboresho hayo ni kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma kwa kupunguza urasimu usio wa lazima, kuimarisha uwajibikaji wa taasisi na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Maboresho haya yataimarisha utendaji wa taasisi mbalimbali kwa kuhakikisha taratibu zisizo za lazima zinaondolewa, hivyo kuongeza ufanisi na kujenga imani ya wananchi katika mifumo ya Serikali,” alisisitiza.
Kwa upande wa uchumi, Bw. Mandepo alisema maboresho ya sheria yatachangia kujenga mazingira salama na yenye uhakika kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Alisema kuwa uwepo wa sheria zinazotabirika, rafiki kwa biashara na zinazoendana na uchumi wa kisasa utachochea ukuaji wa sekta ya viwanda, uwekezaji, biashara na uchumi wa kidijitali.
Katika sekta ya haki, alisema maboresho hayo yanalenga kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati, kwa gharama nafuu na kwa usawa.
“Lengo letu ni kuwa na mfumo wa haki unaomfikia kila mwananchi kwa urahisi, unaozingatia usawa na unaoendana na mahitaji ya jamii inayobadilika,” alisema.
Aidha, Bw. Mandepo alieleza kuwa Serikali imeona umuhimu wa kuwa na mfumo endelevu wa kupitia na kutathmini sheria ili kuhakikisha hazipitwi na wakati kutokana na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia.
Alisema maboresho yanayoendelea yatawezesha Tanzania kuwa na sheria zinazokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye, na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa mujibu wa Bw. Mandepo, sheria bora zitakuwa nguzo muhimu katika kujenga taifa lenye utawala bora, uchumi imara, mazingira rafiki ya uwekezaji na huduma bora kwa wananchi.