Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

Katibu Mtendaji Wa Tume ya Kurekebisha Sheria: Maboresho ya Sheria Yamelenga Kuchochea Uchumi Wa Taifa
26 Nov 2025
Katibu Mtendaji Wa T...

Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRC), Bw. George Mandepo, amesema kuwa maboresho mbalimbali ya sheria yanayoendelea kufanywa na Tume yamelenga kuimarisha uchumi wa taifa na kuweka mazingira wezeshi kwa ukuaji wa sekta mbalimbali za maendeleo.

Akizungumza leo tarehe 26.11.2025  jijini Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa tume hiyo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa tume hiyo kwa waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Juma Zuberi Homera  , Katibu Mtendaji alisema kuwa Tume imekuwa ikifanya mapitio ya kina ya sheria zilizopitwa na wakati ili kuziweka katika hali inayokidhi mahitaji ya dunia ya sasa inayokua kwa kasi, hususan katika maeneo ya biashara, teknolojia na uwekezaji.

“Maboresho ya sheria tunayofanya hayalengi tu kuimarisha mfumo wa kisheria, bali pia kuchochea uchumi wa taifa. Tunataka sheria ziwe sehemu ya suluhisho la kuvutia uwekezaji na kuongeza ushindani wa nchi katika masoko ya kimataifa,” alisema Katibu Mtendaji.

Alibainisha kuwa mfumo thabiti wa sheria ni injini muhimu ya maendeleo ya kiuchumi kwa kuwa unatoa uhakika kwa wawekezaji, unarahisisha upatikanaji wa haki, na kuimarisha mazingira ya biashara.

Bw. Mandepo aliongeza kuwa Tume imekuwa ikifanya tafiti na kuhusisha wadau ili kuhakikisha sheria mpya na zilizoboreshwa zinakuwa za kisasa na za kutekelezeka.

Katika kikao hicho, Katibu Mtendaji alitaja baadhi ya maeneo yanayopewa kipaumbele katika maboresho hayo kuwa ni pamoja na sheria za uwekezaji, biashara, ardhi, ajira, mazingira na masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano.

“Lengo letu ni kuifanya Tanzania kuwa na sheria rafiki kwa maendeleo, zinazohamasisha ubunifu, na kuwezesha uchumi kukua kwa kasi na kwa manufaa ya wananchi wote,” aliongeza.

Viongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria waliipongeza Tume kwa jitihada hizo, wakisema kuwa maboresho hayo ni muhimu katika safari ya nchi kuelekea uchumi wa kati na wa kisasa.

Katibu Mtendaji alihitimisha kwa kusisitiza kuwa Tume itaendelea kufanya kazi kwa weledi, utafiti wa kina na ushirikishwaji mpana wa wadau ili kuhakikisha kuwa mfumo wa sheria unaendana na mabadiliko ya kimataifa na mahitaji ya Taifa kwa ujumla.