Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

DC. MUSSA KILAKALA AIOMBA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA KUFUNGUA TAWI MOROGORO.
24 Nov 2025
DC. MUSSA KILAKALA A...

Mkuu wa wilaya ya Morogoro Mh. Mussa R. Kilakala, ameomba Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, kuweka tawi la ofisi yao Manispaa ya Morogoro ili kusaidia wananchi elimu ya kisheria kuhusu changamoto mbalimbali za kisheria wanazopitia.

Mhe.Kilakala aliyasema hayo Novemba 24, 2025 alipotembelea banda la Tume hiyo katika Maonesho ya kibiashara yaliyoratibiwa na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) yanayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Akizungumza kueleza kuhusu changamoto za kisheria zinazowakabili wananchi wa Morogoro, Mkuu huyo wa Wilaya alisema kumekua na wimbi kubwa la migogoro ya wakulima na wafugaji ambao usuluhishi wake ni kupatiwa elimu ya kisheria ambapo alieleza wengi wao hawana ufahamu, jambo linalopelekea migogoro hiyo kujirudia rudia.

"Sisi hapa tuna Wafugaji na Wakulima wana migogoro ya kisheria kila siku nadhani Tume mlitakiwa muwe na tawi hapa kutusaidia kuwaelimisha" alisema Mh. Kilakala.

Afisa Sheria kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Bi. Jackline Nungu, alisema licha ya kutokua na tawi mkoani hapo bado wananchi wanayo nafasi ya kutumia kipindi hiki cha maonesho kufika bandani hapo kujifunza kuhusu sheria mbalimbali na kueleza kuwa Tume hushiriki katika kampeni na maonesho mbalimbali ili kutoa elimu ya sheria na msaada wa sheria kwa wananchi.

Aidha Jackline aliongezea kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia ya habari na mawasiliano, Tume imekua ikitoa elimu kupitia  vyombo vya Habari kama vile, vituo vya redio, televisheni na Magazeti na kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa pamoja.

Aidha alieleza kuwa wananchi pia wanaweza kuwafuatilia kupitia tovuti, na anuani za mitandao ya kijamii ili kuendelea kuchangia na kutoa maoni yao ya mapendekezo ya marekebisho ya sheria mbalimbali.

"Tunazo anuani zetu wananchi pia wanaweza kutufuatilia na kutoa maoni tovuti yetu ni www.lrct.go.tz , na kwa mitandao ya kijamii instagram na facebook ni tumesheria.tanzania"  alimaliza akieleza Jackline.

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inashiriki Maonesho ya Kibiashara Mkoani Morogoro kwa ajili ya kutoa elimu ya sheria kwa Umma ambapo Maonesho hayo yalianza Novemba 20, 2025 na kutegemewa kuhitimishwa Novemba 30, 2025.