Tume Yaanza Utafiti wa Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeanza kufanya utafiti wa kupitia Mfumo was Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi. Utafiti huo unafuatia kubainika upungufu ambao ni kikwazo katika hifadhi ya taarifa binafsi. Moja ya upungufu ni baadhi ya masharti ya sheria hizo kugongana na kushindwa kuleta ufanisi katika utekelezaji wake.
Kwa kuzingatia kifungu cha 9(1) cha Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Tume na Wizara ya Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano zinafanya utafiti huo kwa kuangalia hali halisi ya utekelezaji wa sheria zilizopo, maoni kuhusiana na sheria inayopendekezwa, udhaifu katika masharti ya sheria zilizopo na maeneo ya sheria yatakayoathirika kutokana na mapendekezo ya kutungwa Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi.
Vile vile, utafiti huo unafanywa kwa kuangalia sheria zikazohitaji kuhuishwa ili kuondoa mgongano kwa lengo la kuenda sambabamba na Sera ya Taifa ya Teknolojia ya Habari pamoja na uundwaji wa idara inayojitegemea ndani ya Mamlaka ya Mawasiliano itakayosimamia ulinzi wa taarifa binafsi.
Tume imewaomba watu binafsi, taasisi za serikali na binafsi kushiriki katika kutoa maoni na mapendekezo kuhusu masuala au masharti yatakayopaswa kuzingatiwa katika Sheria ya Kulinda Taarifa Binafsi.

Powered by WordPress | Designed by: Premium WordPress Themes | Thanks to Themes Gallery, Bromoney and Wordpress Themes