HOTUBA YA MGENI RASMI MH. JAJI ALOYSIUS MUJULIZI MWENYEKITI WA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA (T) KWENYE UFUNGUZI WA KIKAO CHA TISA CHA BARAZA LA WAFANYAKAZI KATIKA HOTELI YA TANGA BEACH RESORT MKOANI TANGA 17-18 SEPTEMBA 2013

Mwenyekiti wa Baraza
Mwenyekiti wa Tawi la TUGHE-TUMESHERIA
Wajumbe wa Baraza
Wageni Waalikwa

Napenda kuwashukuru kwa kunialika kuja kufungua mkutano wa tisa wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na pia nawapeni pole kwa safari ya kutoka Dar es Salaam kufika hapa.

Aidha, naishukuru sana Kamati ya Maandalizi kwa ujumla kwa kufanya maandalizi mazuri na ya uhakika kiasi cha kuwezesha mkutano huu wa Baraza la Wafanyakazi kufanyika leo hapa Tanga. Tukiwa kwenye mandhari nyingine tofauti na ile ya kila siku tuliyozoea.

Ndugu Mwenyekiti wa Baraza,
Nakumbuka tulipokutana kwenye baraza la mwezi April 2013, pale Hoteli ya Giraffe Dar es Salaam kulikuwa na majukumu yaliyoainishwa yaliyohitaji umakini na uharaka katika kuyafanyia kazi hii ikiwa ni pamoja na kukamilisha Mpango Mkakati mpya wa Tume 2013-2018; kuweza kuweka mikakati ya ziada ya kuitangaza Tume yetu ili itambulike na kueleweka shughuli zake na wananchi (increased visibility); kuongeza nguvu katika kutafuta rasilimali zaidi ili kuweza kukabiliana na changamoto zilizopo. Pia umuhimu wa Tume kuanza kujizatiti zaidi kujiandaa upokeaji wa ongezeko la hitaji la mapitio ya sheria mbalimbali hasa ikizingatiwa kuwa Taifa letu lipo katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Mategemeo yakiwa endapo Katiba mpya itapitishwa ni wazi kutakuwa na hitaji la mabadiliko makubwa katika sheria zetu mbalimbali. Ukiachilia suala la Katiba, sasa hivi kuna eneo linalokuwa na muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu, yaani rasilimali za gesi, mafuta na rasilimali za asili ambapo sisi kama Tume ya Kurekebisha Sheria tunapaswa kujipangia mikakati ya mchango wetu katika eneo hili na kujiandaa zaidi kutoa mchango katika kuwezesha uwepo wa mfumo mzuri wa sheria na haki, tukizingatia mamlaka na uwezo wetu. Yoye haya bado tunahitaji kuyaangalia kwa undani na upana wake.

Ndugu Mwenyekiti wa Baraza,
Kwa mara nyingine nimepewa nafasi ya kukutana nanyi ambao ndio viongozi na wawakilishi wa watumishi katika kutoa maamuzi muhimu ya kuijenga Tume zaidi. Naomba nafasi ya kukutana kama baraza muipokee kama fursa pekee ya kutathmini utendaji wetu sisi watumishi na kuangalia namna ya kuboresha utendaji wetu na pale tunapoona kuwa hatukufanya kwa kiwango kinachotakiwa basi tuaangalie namna gani tunaweza kufanya vizuri.

Pamoja na kutathmini utendaji wetu tukumbuke kuwa mbele yetu kuna jambo kubwa la kihistoria kwa Tume ambapo tunaenda kuadhimisha miaka thelathini ya Tume. Ni wakati muafaka kupima matokeo ya tulikotoka, tulipo na tunakoelekea. Napenda kuchukua fursa hii kuwahimiza kutumia maadhimisho haya kama chachu ya kuitangaza Tume kwa kuueleza umma kuhusu yale ambayo tumeyafanya kwa Taifa letu na wananchi na kuwa kitu kimoja. Tukumbuke kuwa fursa hii ni adimu kuipata, hivyo tutumie nafasi hii kwa ufasaha na hekima kutimiza malengo yetu ya kutaka Tume ifahamike kwa umma.

Ndugu Mwenyekiti wa Baraza,
Nimedokezwa kuwa mbali na mambo mengine, Baraza hili litaangalia Bajeti ya Tume 2013/2014, Rasimu ya Mpango Mkakati wa Tume pamoja na kuwasilishwa kwa mada inayohusiana na mfuko wa Bima ya Afya. Napata faraja kubwa kuwa baada ya kukamilika kwa kazi ya uwasilishwaji wa mada mbalimbali na kufuatiwa na majadiliano ya kina kutoka kwa washiriki wa Baraza la Wafanyakazi nyote kwa pamoja mtakuwa tayari kujitoa kwa dhati katika kutekeleza jukumu kubwa la msingi la Tume ambalo ni kutoa mapendekezo ya marekebisho ya sheria mbalimbali zilizopitwa na wakati kwa serikali.

Bajeti ni nyenzo muhimu katika urekebishwaji wa sheria. Mapitio ya Bajeti ni utekelezaji wa matakwa ya sheria, bajeti ni matokeo ya mipango na bajeti ni nidhamu. Pamoja na kujitathmini wenyewe katika utekelezaji wa ahadi kwa wananchi tunazotoa kupitia bajeti zetu zipo taasisi nyingine za umma zinazotuangalia ili kuhakikisha tuna nidhamu ya matumizi ya fedha, tuna nidhamu katika manunuzi na tuna nidhamu katika kulinda mali ya umma iliyo chini ya dhamana yetu.

Mada kuhusu Mpango Mkakati (SP) wetu mpya, ni muhimu kwa sababu unaweka utaratibu wa mpangilio wa kutimiza majukumu ya kurekebisha sheria. Mpango kama huu unahitaji nidhamu, tukielewa kupanga ni kuchagua. Rasilimali watu na fedha ni adimu ili tuweze kupimwa na kuwajibika kwa wananchi lazima tujizatiti katika kile tunachokipanga kuweza kutekeleza kwa ufanisi wa hali ya juu shughuli zilizoainishwa kisheria kama kazi na majukumu ya Tume. Na kutimiza matarajio ya wananchi kwetu, Ni budi pia kuzingatia umuhimu ya kuwa na matokeo mapema (Big Results Now!).

Nimedokezwa zaidi kuwa kutakuwa na Mada kuhusu masuala ya Bima ya Afya, suala hili ni jambo muhimu sana, hasa kwakuwa linalenga ustawi wa mtumishi na familia yake kiafya. Afya njema inasaidia mtu kuwajibika na kutimiza majukumu yake ya kila siku kwa ari na nguvu zaidi. Hivyo basi ni matumaini yangu kuwa katika mada hii wajumbe watapata fursa kupata elimu, uelewa na stadi zaidi katika eneo hili, pamoja na kujadiliana kwa kina mambo yanayohusu mfuko huo na mwisho kuondoa hofu yoyote iliyokuwepo kuhusiana na huduma zinazohudumiwa na mfuko huo.

Ndugu Mwenyekiti wa Baraza,
Naamini kuwa baada ya mkutano huu wa Baraza la Wafanyakazi tutakuwa tayari kutekeleza kwa ueledi mkubwa kazi za Tume kisheria ambazo baadhi na za msingi ni:

• Kuchunguza sheria yoyote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nia ya kuendelea kuiborresha.
• Kupitia sheria au tawi la sheria na kupendekeza hatua muhimu ili kuifanya sheria hiyo iendane na mazingira ya sasa ya Tanzania.
• Kupendekeza njia sahihi za usimamizi wa sheria na haki.
• Kurahisisha ili kuwawezesha wananchi walio wengi kuzielewa sheria mbalimbali zilizopo na zinazotumika nchini.

Ndugu Mwenyekiti wa Baraza,
Kwa kuzingatia majukumu haya ya kisheria ambayo Tume inayo , kupitia mkutano huu wa tisa wa Baraza la Wafanyakazi TUMESHERIA napenda kutoa rai yangu ya kutaka Tume kuhakikisha tunaweka mikakati bora ya kuweza kutekeleza majukumu yake ya kisheria kwa ufanisi zaidi na kwa wakati tukuzingatia ueledi, rasilimali na taaluma zilizopo.

Mwisho, naomba kurudia tena kuwashukuru kwa kupata fursa hii muhimu ya kuzungumza nanyi machache nikiwa kama mwalikwa na kuweza kufungua mkutano wa tisa wa Baraza la wafanyakazi TUMESHERIA . Kwa kupitia kikao hiki nirudie kusema nipo tayari wakati wowote mkinihitaji kushirikiana na menejimenti pamoja na watumishi wote wa Tume kwa lengo la kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Tume.
Baada ya kusema hayo machache sasa nachukua fursa hii kutamka kuwa mkutano wa tisa wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania umefunguliwa rasmi.

Nawatakia mafanikio mema katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kazi.

MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI TUMESHERIA

Powered by WordPress | Designed by: Premium WordPress Themes | Thanks to Themes Gallery, Bromoney and Wordpress Themes