Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania yabidhi Taarifa ya Mapitio ya Mfumo wa Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi tarehe 17 Mei 2014

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania yakabidhi ripoti ya utafiti wa utatuzi wa migogoro ya ardhi Tanzania kwa Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dk Asha Rose Migiro (Mb) tarehe 17 Mei 2014 mkoani Dodoma.

Makabidhiano ya Ripoti hiyo yanafuatia kukamilika kwa mapitio na utafiti wa sheria zinazosimamia utatuzi wa migogoro ya ardhí katika mikoa nane ya Tanzania Bara, wilaya 17 na kata  3 kuanzia ngazi ya kijiji mpaka mkoa.

Katika utafiti wake Tume iliwahusisha wadau mbalimbali wakiwemo wanasheria, Mahakama, Wizara ya Ardhi, Taasisi zisizokuwa za kiserikali (Ngos) pamoja na mabaraza ya kijiji, kata na mkoa. Kutokana na geografia ya nchi Tume ilijigawa katika  mikoa kulingana na Kanda ambazo ni  Kanda ya Ziwa –Mwanza, Geita na Kagera (Chato na Bukoba), Kaskazini- Arusha (Monduli na Arumeru ) & Manyara (Babati na Hanang), Nyanda za Juu Kusini  Iringa (Iringa na Njombe) & Mbeya (Mbeya na Mbarali) na Kanda ya Mashariki –  Dar es salaam  (Ilala na Kinondoni) & Morogoro (Morogoro na Kilosa).

Tume iliona umuhimu wa kuangalia eneo hili ambalo limekuwa linalalamikiwa sana na wananchi ili kutoa mapendekezo ya namna Sheria hiyo inavyoweza kurekebishwa, kuondoa kasoro za kisheria na kiutekelezaji zilizojitokeza pamoja na malengo na makusudio ya Sheria hiyo yaweze kutekelezwa kwa ubora na mafanikio zaidi kama ilivyotarajiwa.

Mnamo mwaka 1999 zilitungwa sheria mbili za ardhi, nazo ni Sheria ya Ardhi Na. 4 ya 1999 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya 1999. Sheria hizo zilitungwa kufuatia Taarifa ya Shivji ya mwaka 1992 na Sera ya Ardhi ya mwaka 1995. Sera ya Ardhi, 2005 inasisitiza juu ya kuanzishwa kwa mahakama maalum za ardhi zitakazohakikisha kuwa utatuzi wa migogoro ya ardhi unakuwa wa haraka na wa haki. Sheria hizi za ardhi, pamoja na mambo mengine, zilianzisha mahakama maalum za ardhi, ambazo ni Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji, Mabaraza ya Kata, Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, Mahakama Kuu na Makahama ya Rufaa. Hizi Sheria zilifuatiwa na Sheria ya Mahakama ya Migogoro ya Ardhi ya mwaka 2002, ambayo iliweka utaratibu wa uanzishwaji wa Mahakama hizo za Ardhi, ikiwemo utaratibu wa kufuata pindi kunapokuwa na migogoro ya ardhi.

Ikiwa ni zaidi ya miaka 10 baada ya uanzishwaji rasmi wa mahakama hizi, Tume  ya Kurekebisha Sheria   imeona  ni muda muafaka wa kupima ufanisi wa taasisi hizo juu ya dhamana kubwa ya kutatua migogoro ya ardhí ambapo Ardhi ni msingi wa maisha ya mwanadamu. Tume imeamua kufanya utafiti katika eneo hili ili  kutathmini  utekelezaji wa sheria hizi na kubaini mapungufu yanayojitokeza wakati wa kutekeleza sheria hizo na kutoa mapendekezo kwa serikali kwa lengo la kuondoa dosari za kisheria na kiutekelezaji zilizojitokeza, ili malengo na makusudio ya Sheria hiyo yaweze kutekelezwa kwa ubora na mafanikio zaidi kama ilivyotarajiwa.

 

Kwa kurekebisha na kuboresha mfumo wa sheria zinazosimamia utatuzi wa migogoro ya ardhi serikali itakuwa imefikia malengo yafuatayo:

  • Utatuzi na usuluhishi wa migogoro ya Ardhi mapema iwezekanavyo utachangia pia kuongezeka kwa ufanisi katika Nyanja za kiuchumi kwa wananchi;
  • Utatuzi na usuluhishi wa migogoro ya Ardhi mapema iwezekanavyo utadumisha ushirikiano na amani kati ya wakulima na wafugaji na serikali kwa ujumla.
  • Maamuzi ya haraka na kwa wakati yataondoa tatizo la urasimu uliopo, vikwazo na mlundikano wa kesi.
  • Itapunguza gharama za kiutawala kwa kuwa na Wizara moja itakayosimamia utatuzi wa migogoro ya ardhi.

 

 

Powered by WordPress | Designed by: Premium WordPress Themes | Thanks to Themes Gallery, Bromoney and Wordpress Themes