TUME YA KUREKEBISHA SHERIA (T) YATANGAZA RIPOTI YA MAPITIO YA MFUMO WA SHERIA ZINAZOHUSU UTATUZI WA MIGOGORO YA ARDHI KATIKA MIKOA YA TANZANIA BARA

Mwaka 1999 zilitungwa sheria za ardhi, nazo ni Sheria ya Ardhi [Na. 4 ya 1999] na Sheria ya Ardhi ya Vijiji [Na. 5 ya 1999].  Sheria hizo zilitungwa kufuatia Taarifa ya Shivji ya mwaka 1992 na Sera ya Ardhi ya mwaka 1995.  Sera ya Ardhi, 2005 inasisitizia juu ya kuanzaishwa kwa mahakama maalum za ardhi zitakazohakikisha kuwa utatuzi wa migogoro ya ardhi unakuwa wa haraka na wa haki.  Sheria zilizotajwa hapo juu, pamoja na mambo mengine, zilianzisha mahakama maalum za ardhi ambazo ni: Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji, Mabaraza ya Ardhi ya Kata na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya.  Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa zilitajwa pia katika utaratibu wa mabaraza hayo.  Hizi sheria zilifuatiwa na Sheria ya Mahakama ya Migogoro ya Ardhi ya 2002, ambayo iliweka utaratibu wa uanzishwaji wa Mahakama hizo za Ardhi.

 

Ikiwa ni miaka zaidi ya kumi baada ya uanzishwaji rasmi ya mahakama hizi, Tume iliona umuhimu wa kufanya utafiti ili kupima ufanisi wa taasisi hizo juu ya dhamana kubwa walilopewa la kutatua migogoro ya ardhi.

 

Tume ilifanya utafiti huu kuhusiana na mahakama hizi katika mikoa nane ya Tanzania Bara mwaka 2011.  Mwaka 2012 Tume ilipita tena katika mikoa hiyo kwa lengo la kuhakiki taarifa ya utafiti iliyokuwa inaonesha mapungufu yaliyoko kwenye sheria husika kama yalivyoainishwa na wadau hao wakati wa utafiti, na mapendekezo ya namna ya kuboresha mapungufu hayo.  Mwaka huu 2013, Tume inapojiandaa kukamilisha ripoti ya utafiti wake, imeandaa vipeperushi na vipindi vya redio kuhusiana na utafiti huu ili kuwapa taarifa wadau juu ya kazi hii ya Tume.

Katika kuwapa taarifa wadau Tume imetembelea mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Iringa, Ruvuma, Lindi na Mtwara Lengo kuu ikiwa ni kutoa taarifa ya utafiti kwa njia ya kusambaza vipeperushi mkoani na wilaya zote za mikoa hiyo pamoja na kurusha kipindi kimoja cha redio katika moja ya mikoa iliyotembelea ambapo Radio ya Triple A Fm- Arusha,  Standard Radio Fm- Singida, Info Radio Fm- Mtwara na Radio Jogoo Fm -Ruvuma zilitumika katika kurusha vipindi.

 

 

Powered by WordPress | Designed by: Premium WordPress Themes | Thanks to Themes Gallery, Bromoney and Wordpress Themes